Idadi ya waathirika wanaoaminika kufa na njaa kutokana na imani kali ya Kikristo nchini Kenya imeongezeka na kufikia 98 hadi kufikia leo mchana, huku familia zingine zikisubiri habari za wapendwa wao ambao ni wafuasi wa kanisa hilo na hadi sasa hawajulikani waliko.
Kupatikana miili karibu 100 iliyokuwa imezikwa katika msitu wa Shakahola karibu na mji wa pwani wa Malindi, Kaunti ya Kilifi kumewashtua wengi Kenya na duniani kote.
Waliofariki walikuwa ni wafuasi wa pote la Kikristo lenye misimamo kali linaloongozwa na mhubiri mwenye utata Paul Mackenzie Nthenge ambaye sasa amekamatwa na anakabiliwa an mashtaka ya kuwahubiria wafuasi wake kwamba kukaa na njaa ndiyo njia pekee ya kwenda kukutana na 'Yesu'.
Kashfa hii ya kuogofya, ambayo imepewa jina la "Mauaji ya Kutisha ya Msitu wa Shakahola", imesababisha msako kuanzishwa kuhusu makanisha ya siri nchini Kenya.
Mashirika ya kutetea haki za kibinadamu sasa yanazilaumu asasi za kiserikali mjini Malindi katika Kaunti ya Kilifi kwa kutomkabili mapema mhubiri huyo wa Kikristo mwenye misimamo mikali. Shirika la Haki Africa sasa limetoa wito kwa serikali kupitia vyombo vya dola kulipa kipaumbele suala hilo ipasavyo na kuhakikisha kuwa maafisa zaidi wa usalama wanatumwa katika eneo hilo.
Rais William Ruto amemtaja mhubiri Paul Mackenzie kama mhalifu na gaidi kufuatia kufukuliwa kwa maiti kutoka kwa ardhi yake huko Kilifi.
Akiongea mjini Kiambu mapema Jumatatu Ruto ambaye alionekana mwenye hasira aliwasuta vikali wachungaji wa Kikristo ambao wamekuwa wakitumia imani potofu za kidini kuwapotosha Wakenya.
Chanzo #Parstoday.