Pichani ni zoezi la kukabidhi mabango katika Ofisi za Uhamiaji Mkoani Kagera.
Uelimishaji juu ya tahadhari na kujikinga ugonjwa wa Marburg ukifanyika katika gulio la Kyamulaile Wilayani Bukoba Mkoani Kagera.
Darasa la namna ya Kukabiliana na Magonjwa ya mlipuko kwa Valontia 80 wa Tanzania Redcross Society limefanyika katika halmashauri ya Muleba , Bukoba Mjini, Kyerwa na Missenyi.
Mwakilishi kutoka Wizara ya Afya Said Makora akiwa Moja ya redio ya kijamii Wilayani Bukoba Mkoani Kagera akitoa elimu jinsi ya kuchukua tahadhari na kujikinga na ugonjwa wa Marburg.
Pichani ni zoezi la uwekaji wa Mabango ya uelimishaji juu ya Marburg kwenye magari maalum ya matangazo yenye ujumbe usemao"Jikinge na Marburg, Iweke jamii yako Salama".
Na.Elimu ya Afya Kwa Umma.
Serikali kupitia Wizara ya Afya, Idara ya Kinga Sehemu ya Elimu ya Afya Kwa Umma imeendelea na afua mbalimbali za uelimishaji kuhakikisha jamii na Taasisi zinakuwa na uelewa wa pamoja katika kuchukua tahadhari na kujikinga ugonjwa wa Marburg .
Miongoni mwa mikakati ambayo imekuwa ikifanyika ni pamoja na kusambaza vipeperushi na mabango ambapo leo April.5.2023 Wizara ya Afya, Idara ya Kinga, Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma Kwa kushirikiana na Ofisi ya Mganga Mkuu wa mkoa imeweza kusambaza mabango katika Ofisi ya uhamasishaji mkoa wa Kagera pamoja na kituo cha polisi Bukoba .
Mabango hayo yana ujumbe Mahsusi kuhusu namna ya kuchukua tahadhari na kujikinga na kutambua dalili mbalimbali za ugonjwa wa Marburg ikiwa ni pamoja homa, maumivu ya kichwa,maumivu ya misuli,kuharisha, mwili kuishiwa nguvu, vidonda vya koo, vipele vya ngozi, maumivu ya tumbo, kutapika.
Dalili zingine ni kutokwa na damu sehemu za wazi kama vile puani,kutapika damu pamoja na kuhara damu.
Mabango hayo yatawekwa katika sehemu mbalimbali ambapo itakuwa rahisi mwananchi kupata elimu kupitia ujumbe uliopo pia yatakuwa yanatumika katika mikutano mbalimbali ya taasisi hizo.
Mbali na zoezi hilo kufanyika ,pia zoezi la kuweka mabango(branding) kwenye magari maalum ya matangazo yatakayotumika kwa ajili ya uelimishaji juu ya tahadhari ya kujikinga na ugonjwa wa Marburg limeendelea katika Mkoa wa Kagera.
Halikadhalika, uelimishaji juu ya tahadhari ya kujikinga na ugonjwa Marburg kwa njia ya redio za kijamii umeendelea katika redio mbalimbali za kijamii zilizopo Mkoani Kagera.
Pia,Uelimishaji juu ya tahadhari na kujikinga ugonjwa wa Marburg umefanyika katika maeneo mbalimbali yenye mikusanyiko ya watu ikiwemo gulio la Kyamulaile Wilayani Bukoba Mkoani Kagera.
Sanjari na hayo,darasa la namna ya Kukabiliana na Magonjwa ya mlipuko kwa Valontia 80 wa Tanzania Redcross Society limefanyika katika halmashauri ya Muleba , Bukoba Mjini, Kyerwa na Missenyi.
Wizara inafanya jitihada zote hizo, ni katika kuhakikisha kila mwananchi anakuwa na tahadhari ya kujikinga mapema kabla ya tatizo halijatokea kwani Kinga ni Bora kuliko Tiba,na Mtu ni Afya.




