Na Gideon Gregory, Dodoma.
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt.John Mduma amesema kuwa jumla ya shilingi bilioni 44.6 zimelipwa na Mfuko huo kwa wanufaika wake kama mafao ikiwa ni ongezeko kubwa ikilinganishwa na kipindi cha kabla ya kuanza kwa Mfuko.
Dkt. Mduma ameyasema hayo leo Machi 2,2023 Jijini Dodoma wakati akielezea utekelezaji wa majukumu ya Mfuko huo katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita mbele ya waandishi wa habari waandishi ambapo amesema kuwa hadi kufikia Juni 30,2022 WCF ilikuwa imelipa mafao hayo kwa wanufaika mbalimbali huku ongezeko kubwa la waajiri kujisajili katika mfuko huo hasa katika kipindi cha awamu ya sita kutokana na hatua za makusudi za kuweka vivutio vya kibiashara na kuondoa vikwazo vilivyokuwepo na kupunguza viwango vya uchangiaji na kutoa msamaha wa riba.
Aidha amefafanua kuwa mfuko huo ulianza rasmi kukusanya michango kwa waajiri tangu Julai mosi mwaka 2015 ambapo hadi kufikia Juni 30 mwaka jana makusanyo yalifikia sh.bilioni 545.4.
“Katika makusanyo hayo sh.bilioni 88. zilikusanywa mwaka wa fedha 2020/2021 na sh.bilioni 86.6 zilikusanywa mwaka wa fedha 2021/2022, makusanyo ya michango ya waajiri yalishuka katika mwaka wa fedha 2021/2022 kutokana na kushuka kwa asilimia ya kiwango cha uchangiaji kwa waajiri wa sekta binafsi kutoka asilimia moja hadi 0.6,”amesema.
Amesema kwa takwimu za mwaka 2016/17, WCF ililipa fidia kwa wanufaika takribani 538 na kiasi cha sh. milioni 613.8 kililipwa huku mwaka 2021/2022 pekee, WCF ililipa fidia kwa wanufaika takribani 1,600 na kiasi cha zaidi ya sh. bilioni 9.33 kililipwa.
Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) ni taasisi ya hifadhi ya jamii iliyoanzishwa chini ya kifungu cha 5 cha Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi (Sura 263) kwa lengo la kulipa fidia kwa wafanyakazi wanaopata ulemavu au kufariki kutokana na magonjwa au ajali zitokanazo na kazi wanazozifanya kwa mujibu wa mikataba yao ya ajira.