WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema kuwa jukumu la usalama barabarani ni la kila mtu na si la Serikali pekee na amewataka wananchi wote watoe ushirikiano kuzuia ajali za barabarani.
Ametoa kauli hiyo jana (Jumanne, Machi 14, 2023) wakati akizungumza na washiriki waliohudhuria uzinduzi wa Wiki ya Usalama Barabarani Kitaifa uliofanyika kwenye viwanja vya Furahisha, jijini Mwanza.
Amesema kuwa madereva wa magari na pikipiki nao wamekuwa ni sehemu kubwa ya vyanzo vya ajali za barabarani na kuchangia kuongezeka kwa ajali kwa kuendesha kwa mwendo kasi, kuyapita magari ya mbele bila ya kuchukua tahadhari, kuendesha magari mabovu ama kutoheshimu alama na michoro ya barabarani.
Katika kuhakikisha ushirikiano miongoni mwa wadau unakuzwa na mapambano dhidi ya ajali za barabarani yanaimarishwa, Waziri Mkuu ameliagiza Baraza la Taifa la Usalama Barabarani liharakishe mchakato wa mapendekezo ya marekebisho ya sheria na kanuni za usalama barabarani ili kuwe na sheria bora isiyoacha mwanya kwa watumiaji wa barabara na waendesha vyombo vya moto.
