Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) nchini wametakiwa kuwa makini wakati wa utekelezaji wa miradi ya miundombinu ya barabara ili utekelezaji huo usiathiri upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii.
Hayo yamebainishwa Machi 14,2023 na Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa( TAMISEMI) Mhe. Denis Londo wakati wa ziara ya kamati hiyo ya kukagua ujenzi wa barabara ya Bujora iliyopo katika Halmashauri ya Magu Mkoa wa Mwanza.
Amebainisha kuwa wakati wa utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu ya barabara katika baadhi ya maeneo nchini umeathiri upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii hasa uharibifu wa miundombinu ya maji.
" Utekelezaji wa miundombinu ya barabara usiharibu miundombinu mingine muhimu katika jamii hakuna sababu ya kukata mabomba na kuwasababishia wananchi adha ya upatikanaji wa maji" Ameeleza Mhe. Londo.
Aidha ameitaka Halmshauri ya Magu kuongeza kasi katika ujenzi wa barabara ya Bujora na ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Mwanza ili miradi hiyo ianze kutoa huduma kama ilivyokusudiwa.
Naye mjumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge TAMISEMI Mhe.Magreth Sitta ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Magu kwa usimamizi mzuri katika utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa shule ya Sekondari ya wasichana Mkoa wa Mwanza,amewataka kuongeza kasi ili kukamilisha sehemu iliyobaki.
Kwa upande wake Naibu Waziri anayeshughulikia Elimu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa , Mhe. Deogratius Ndejembi ameihakikishia Kamati ya kudumu ya TAMISEMI kuwa maagizo yote yaliyotolewa yatafanyiwa kazi kama yaliyoelekezwa na kamati hiyo.

