Na Gideon Gregory, Dodoma.
Kufuatia janga la Kimbuga kiitwacho TROPIKI FREDDY kilichoipiga nchi ya Malawi na kusababisha madhara makubwa, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa misaada mbalimbali ya kibinadamu kwa nchi hiyo ili kusaidia kukabiliana na janga hilo.
Hayo yamebainishwa leo Machi 18,2023, jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Habari na uhusiano wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Luteni Kanali Gaudentius G. Ilonda mbele ya waandishi wa habari ambapo ametaja misaada hiyo kuwa ni shehena ya chakula Tani 150, Mablanketi, Mahema na mahitaji mengine yanayotelewa na Serikali.
“ Kufuataia jukumu hilo mkuu wa majeshi Jenerali Jacob John Mkunda, ametoa maelekezo yanayoratibiwa na Manadhimu mkuu wa JWTZ Luteni Jenerali Salum Haji Othman, magari ya JWTZ zaidi ya 37 yataondoka Dodoma muda wowote kuanzia hivi sasa kupeleka misaada nchini Malawi,”amesema.
Luteni Kanali Ilonda amesema magari hayo yanayopelekwa Malawi ni pamoja na gari la wagonjwa, karakana ya magari inayotembea na malori makubwa 20 yenye uzito wa tani 30 na malori zaidi ya 10 yenye uzito wa tani 10.
Aidha ameomgeza kuwa JWTZ litapeleka Helikopita mbili ikiwa ni sehemu ya msaada uliotolewa na Serikali kuisaidia Malawi kukabiliana na janga hilo.
“Kimbunga hicho kimesababisha maafa makubwa kiasi cha kutangazwa kuwa janga nchini humo baada baada ya kusababisha vifo, kuharibu miundombinu, nyumba, mazao na athari nyingine kadha wa kadha,”ameongeza.
