Greyson Mwase na Mwanahamisi Msangi, Arusha.
Kamishna wa Madini kutoka Wizara ya Madini, Dkt. Abdulrahman Mwanga amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Madini itaendelea kutatua changamoto kwa watoa huduma kwenye shughuli za utafiti na uchimbaji wa madini ili kuhakikisha watanzania wote wananufaika na uwekezaji katika Sekta ya Madini ili sekta hiyo iendelee kuwa na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi.
Dkt. Mwanga ameyasema hayo leo Machi 15, 2023 kwenye Jukwaa la Pili la Utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini linaloendelea jijini Arusha linalokutanisha kampuni za uchimbaji wa madini, watoa huduma wa madini kwenye migodi ya madini na Taasisi za Kifedha.
Amesema kuwa ili kuhakikisha watanzania wote wananufaika na rasilimali za madini nchini, Serikali imeendelea kuboresha Sheria za Madini ikiwa ni pamoja na Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na marekebisho yake ya mwaka 2017 yenye lengo la kuhakikisha kila mtanzania kwa namna moja ama nyingine anashiriki kwenye uchumi wa madini.
Amesema kuwa, kama mkakati wa kutatua changamoto za watoa huduma kwenye migodi ya madini, Serikali kupitia Tume ya Madini imekuwa ikitoa elimu kwa wadau wa madini ikiwa ni pamoja na majukwaa mbalimbali yenye lengo la kubadilishana uzoefu, kujadiliana changamoto mbalimbali pamoja na kuzitatua.
Katika hatua nyingine, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa mstari wa mbele kwa uhamasishaji wa Serikali kuendelea kufanya kazi na Sekta Binafsi na kuongeza kuwa Wizara ya Madini chini ya Waziri wake, Dkt. Doto Biteko imeendelea kukutana na wawekezaji binafsi, taasisi za kifedha na kuwaunganisha na kampuni za madini ili kukuza uwekezaji katika Sekta ya Madini.
Aidha, ameipongeza Tume ya Madini kwa mwendelezo wa majukwaa na mikutano mbalimbali ambayo imekuwa ikifanyika mara kwa mara kama lengo la kuelimisha wadau wa madini kuhusu fursa za uwekezaji zilizopo katika Sekta ya Madini.
Wakati huohuo, Mkurugenzi wa Ukaguzi na Biashara ya Madini kutoka Tume ya Madini, Venance Kasiki akielezea lengo la jukwaa hilo amesema kuwa ni kuwakutanisha watoa huduma na kampuni za madini ili kubadilishana uzoefu, fursa zilizopo ili kufungamanisha Sekta ya Madini na sekta nyingine kwa ukuaji wa uchumi wa nchi.
“Kama Tume ya Madini, tutaendelea kuhakikisha wananchi wote wanashiriki kwenye shughuli za uchumi wa madini kuanzia kwenye utafiti, uchimbaji, biashara ya madini na utoaji wa huduma kama vile ajira, vyakula, ulinzi, ili waendelee kunufaika na Serikali kuendelea kupata mapato yake,” amesema Kasiki.
Washiriki wengine walioshiriki katika jukwaa hilo ni pamoja na Makamishna wa Tume ya Madini, Janet Lekashingo na Profesa Abdulkarim Mruma, Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo, Watendaji kutoka Wizara ya Madini na Tume ya Madini, mwakilishi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Arusha na Viongozi wa Dini.


