Mgogoro uliodumu takriban miaka kumi tano (15) baina ya Wakulima na Wafugaji wa Vijiji vya Izava na Chitego mpakani mwa Wilaya za Kongwa na Chamwino umepata suluhu.

Suluhu hiyo imeletwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule  baada ya kuitisha kikao cha maridhiano baina ya pande zote mbili za wakulima na wafugaji waliokuwa wakigombea eneo la malisho na kilimo.

Mhe. Senyamule akiwa katika kitongoji cha Wali Wilaya ya Chamwino, amefanya mkutano wa hadhara na kutoa msimamamo wa Serikali kuwa itachongwa barabara katika eneo linalogombewa itakayoonesha mpaka wa eneo la wakulima na wafugaji.

“Hapa tunataka amani itawale, barabara ile ndio mpaka, itakuwa ni marufuku kwa mkulima kuvuka kwenda kwa mfugaji kwa shughuli za kilimo na pia mfugaji kuchunga eneo la mkulima, maamuzi haya yaheshimiwe na pande zote mbili” Alisisitiza Mhe. Senyamule.

Amewataka wakulima na wafugaji kuhakikisha wanazingatia maazimio waliyoafikiana huku akisema hatua kali zitachukuliwa kwa kiongozi au mwananchi yeyote atakayekwenda kinyume na maelekezo hayo. Pia amekemea vikali tabia ya kujichukulia sheria mkononi kwani ni kinyume cha sheria na ni uvunjifu wa amani.

Aidha, Mhe.Senyamule amekemea suala la viongozi wa vitongoji na vijiji kuuza maeneo bila kuwashirikisha maafisa ardhi akidai kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.

"Kwa sheria ya nchi yetu kitongoji hakimiliki ardhi, hakuna Mwenyekiti wakitongoji mwenye haki ya kugawa, kuuza wala kubadili matumizi ya ardhi, ardhi inamilikiwa kuanzia ngazi ya kijiji na kushirikiana na kitongoji, kijiji kinaruhusiwa na kina mipaka yake kina uwezo wakuuza ukubwa wa eneo heka 50 na si zaidi ya hapo na eneo linauzwa na wanakijiji wote kwa makubaliano ya mkutano wa Kijiji" Mhe. Senyamule amebainisha.

 

Mkuu huyo wa Mkoa amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote mbili za Kongwa na Chamwino kuunda kamati ya watu 10 itakayojumuisha wajumbe watano kutoka kila upande ili kuharakisha zoezi la kuweka barabara hiyo na kusikiliza migogoro na changamoto zozote zitakazojitokeza mara baada ya utekelezaji wa maazimio kuanza.

 

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Remidius Mwema anayekaimu pia Wilaya ya Chamwino amesema suluhu ya mgogoro huo imetokana na mapendekezo ya vikao mbalimbali vilivyohusisha pande zote mbili.







Maoni