Na Gideon Gregory, Dodoma.
Kaimu Mkurugenzi wa Habari na uhusiano wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Luteni Kanali Gaudentius G. Ilonda leo Machi 9,2023 ametangaza nafasi za kujiunga na Jeshi hilo kwa vijana wenye umri kuanzia miaka 18 hadi 26 kwa wenye elimu ya kidato cha 4 na cha sita pamoja na walio na miaka 27 kwa wenye elimu ya juu.
Luteni Kanali Ilonda ametoa tangazo hilo mbele ya waandishi wa habari Jijini Dodoma ambapo amesema vijana wenye elimu ya kuanzia kidato cha nne hadi shahada ya uzamili ambao wamemaliza mkataba wa mafunzo ya kujitolea JKT na kurudishwa majumbani ndiyo Wenye sifa za kuomba nafasi za kujiunga na Jeshi hilo.
"Nafasi hizi haziwahusu vijana ambao bado wapo katika kambi mbalimbali za JKT kwa sasa bali zinawahusu wale ambao tayari wamemaliza mikataba yao ya mafunzo ya miaka miwili na kurudishwa majumbani na wenye vigezo vilivyotajwa vya kuomba nafasi hii," amesema.
Aidha amewatahadharisha wananchi kuwa makini na matapeli pindi wanapoanza kutafuta ajira kwani kumekuwa na tabia ya kuibuka matapeli pindi matangazo ya nafasi za kujiunga na jeshi hilo zinapotangazwa.
"Natambua katika matangazo haya ya kujiunga na nafasi hizi kuna matapeli watajitokeza na kuanza kupenyeza utapeli wao ,mara jaza fomu hii kitu ambacho siyo kweli hivyo nawataka watanzania wasidanganyike wala kurubuniwa na hakuna njia ya mkato katika kupata nafasi hizi zaidi ya kuzingatia vigezo vilivywekwa wazi kabisa,'amesema.
Sanjari na hayo, amefafanua namna ya kutuma maombi kuwa maombi yote yaandikwe kwa mkono na yawasilishwe makao makuu ya jeshi hilo Dodoma kwanzia leo Machi ,9 hadi Machi 20, 2023 yakiwa na viambatanisho ambavyo ni nakala ya kitambulisho cha taifa au namba ya nida,nakala ya cheti cha kuzaliwa,vyeti vya shule na chuo,nakala cheti cha JKT na namba ya simu ya mkononi ya muombaji.
Pia ametaja vigezo vitakavyozingatiwa wakati wa maombi hayo kuwa mwombaji awe raia wa Tanzania wa kuzaliwa mwenye kitambulisho cha Taifa,awe na afya nzuri na akili timamu,awe na cheti halisi cha kuzaliwa,vyeti vya shule nav yeti vya taaluma.
“Vigezo vingine awe hajatumikia Jeshi la Polisi,magereza,Chuo cha Mafunzo au Kikosi maalumu cha kuzuia magendo (KMKM) na asiwe ameoa au kuolewa,”amesema.

