Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Adolf Mkenda amesema kuna haja ya Vyuo Vikuu na taasisi za elimu ya juu katika jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuimarisha ushiriki wa sekta ya umma na binafsi katika masuala ya elimu ili kuongeza tija katika utoaji elumu.
Prof. Mkenda amesema sekta binafsi ina nafasi kubwa sana ya kuchangia uboreshwaji wa elimu kuanzia ngazi ya chini hadi elimu ya juu na hivyo kuleta uhalisia wa ushirikiano wa sekta binafsi na umma kwa maendeleo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Prof. Mkenda amesema hayo alipokuwa akifungua kongamano la 12 Elimu kuhusu ushirikiano kati ya vyuo vya kati, vyuo vikuu na sekta ya umma na binafsi, lililoandaliwa na Baraza la Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki (IUCEA) kwa kushirikiana na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) jijini Dar es Salaam linaloenda sambamba na maonyeshi.
Prof. Mkenda ameeleza umuhimu wa kushirikisha sekta binafsi katika kutafuta suluhu ya kudumu kuhusu changamoto za elimu ya juu ikiwemo uandaaji wa mitaala.
Akitoa mfano wa Tanzania, amesema umuhimu wa sekta binafsi umedhihirika kuanzia ngazi ya chini ya elimu hadi vyuo vikuu.
"Jukwaa hili limechagiza mashirikiano katika kuboresha mitaala kwa kushirikiana na sekta binafsi. Kuimarishwa kwa elimu bora kunahitaji sekta binafsi kuwa mshirika wa karibu," amesema Prof. Mkenda huku akibainisha kuwa sekta binafsi inamiliki vyuo vikuu vingi zaidi nchini Tanzania ikilinganishwa na sekta ya umma ingawa vyuo vikuu vya umma vinadahili wanafunzi wengi zaidi.
Aidha, Prof. Mkenda ameiomba IUCEA kuja na mpango maalumu utakaokubaliwa na nchi zote ili kufufua mabadilishano ya wanafunzi wa vyuo vikuu na wafanyakazi wa taaluma kati ya nchi hizo ikiwa ni njia ya kuifanya elimu ya juu kuwa ya kimataifa.
“Tufike mahali sasa mwanafunzi wa Kitanzania awe na uhuru wa kuchagua chuo cha kwenda Afrika Mashariki na sifa zake zitambulike nchini mwake, hii itatusaidia kuendeleza umoja huu wa jumuiya yetu kwa vizazi na vizazi" amesema.
Naye Katibu Mtendaji wa IUCEA, Prof. Gaspard Banyankimbona amebainisha kuwa kongamano hilo limelenga vyuo vikuu kuja na mikakati na mbinu mpya zinazohusisha uanzishaji wa ushirikiano na sekta ya uzalishaji na viwanda.


