Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amesema Serikali haitamvumilia mwajiri yeyote katika taasisi za umma atakayeshindwa kusimamia haki za watumishi kama ilivyoelekezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mhe. Jenista ametoa kauli hiyo katika Halmashauri ya Wilaya ya Siha wakati wa kikao kazi chake na watumishi wa halmashauri hiyo kilicholenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma na kusikiliza changamoto za watumishi hao kwa lengo la kuzitatua.
Mhe. Jenista amesema, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alipoingia tu madarakani kwa mara ya kwanza, aliainisha vipaumbele vyake, ikiwamo kusimamia haki na stahiki za watumishi wa umma, wajibu na kufanya kazi kwa hiari bila kushurutishwa na kuongeza kuwa aliainisha vipaumbele hivyo kwani anaamini rasilimaliwatu ndio rasilimali inayowezesha shughuli zote za serikali kufanyika kwa ufasaha ili kutoa huduma zenye viwango kama ilivyokusudiwa.
Mhe. Jenista amemshukuru Mhe. Rais kwa kuwaamini na kuwateua katika nyadhifa walizonazo yeye pamoja na wasaidizi wake, hivyo anamuahidi kusimamia utekelezaji wa vipaumbele alivyovianisha ili maono yake ya kuwa na utumishi uliotukuka yanafikiwa.
Mhe. Jenista ameongeza kuwa, haki na stahiki zinaendana na wajibu, hivyo kama ambavyo Mhe. Rais ameonyesha kuwajali watumishi wa umma katika kusimamia haki na stahili zao, basi nao hawana budi kuwajibika kikamilifu ili kuhakikisha huduma bora kwa umma zinatolewa.
“Mhe. Rais anatamani kuona kila mtumishi anapenda kufanya kazi kila wakati na bila kushurutishwa ili kutoa huduma bora kwa umma na ndio maana ameweka masilahi yenu mbele, hivyo na mimi na wasaidizi wangu tutahakikisha azma hiyo ya Mhe. Rais inafikiwa,” Mhe. Jenista amesisitiza.
Aidha, Mhe. Jenista amewasisitiza Watendaji kupitia Maafisa Utumishi wao kubeba jukumu la utumishi wao katika kusikiliza na kutatua kwa wakati changamoto zinazowakabili watumishi ili kuwawezesha watumishi kufanya kazi kwa bidii.