WAZIRI MABULA ASISITIZA MAENEO YA UWEKEZAJI KUPANGWA NA KUPIMWA

MUUNGANO   MEDIA
0

 


Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amesisitiza maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli za uwekezaji nchini kupangwa, kupimwa na kumilikishwa kwa lengo la kuepuka migogoro ya ardhi.

Dkt Mabula ametoa kauli hiyo tarehe 23 Februari 2023 katika ofisi ndogo ya Wizara ya Ardhi jijini Dar es Salaam wakati akipewa taarifa ya mradi wa kupanga, kupima na kumilikisha viwanja eneo lenye ukubwa wa ekari 630 lililopo mkabala na mradi wa kuchakata gesi asilia-LNG la Mto Mkavu na Likong’o mkoani Lindi unaotekelezwa na halmashauri ya manispaa ya Lindi.

Waziri Mabula alisema, katika kipindi hiki ambacho Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan anasisitiza suala la uwekeza ni muhimu mamlaka husika kuhakikisha zinapanga, kupima na kumilikisha maeneo ya uwekezaji ili kuwarahisishia wawekezaji wanapokuja kuwekeza nchini.

Akielezea zaidi kuhusu mradi wa kupanga, kupima na kumilikisha viwanja katika eneo la Mto Mkavu na Likong’o mkoani Lindi Dkt Mabula pamoja na kupongeza mradi huo ametaka kuwepo uwazi wakati wa mchakato mzima wa kutangaza viwanja vya mradi huo sambamba na kuepuka mtu mmoja kuchukua viwanja vingi ambavyo mwisho wa siku atashindwa kuviendeleza kwa wakati.

‘’Hatuzuii mtu kuchukua viwanja lakini siyo mtu achukue mtaa mzima halafu anashindwa kuviendeleza na eneo kubaki vichaka, mimi sitotaka kusikia jambo hilo katika kipindi changu cha uongozi hapa wizara ya ardhi’’ alisema Dkt Mabula.

Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)