Shirikisho la Vyuo vya Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO) wameipongeza Serekali kwa kudhamiria kuja na Muswada wa Bima ya Afya kwa Wote ambao unategemewa kusomwa Bungeni tarehe 09 hadi 10 mwezi huu.
Wakiongea kwa nyakati tofauti kwenye mkutano Mkuu wa Seneti Kitaifa ambao unajumuisha Ma-Rais na Viongozi mbalimbali wa Serikali za wanafunzi wa Vyuo Vikuu nchini unaofanyika jijini Mbeya wamesema ujio wa Muswada wa Bima ya Afya kwa Wote utasaidia wanafunzi pamoja na familia zao kuwa na uhakika wa matibabu pale wanapougua bila kikwazo cha fedha pamoja na ukuaji wa uchumi kwa mtu mmoja mmoja kutokana na kupunguza mzigo wa gharama wa matibabu wakati wote.
Yolanda Kimata Rais wa Chuo Kikuu cha Ardhi na Hoseni Abdala Rais wa Chuo cha Elimu ya Biashara Dodoma wameeleza kuwa baada ya kupatiwa elimu hii ya Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote wanaipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa Mhe. Dkt. Samia S Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kujali afya za Watanzania katika maboresho ya vituo vya afya na kusema kuwa ujio wa mswaada huu utaleta usawa kwenye utoaji wa matibabu.
Naye Felista Joseph Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Afya na Mazingira TAHLISO amesema kwa sasa Tanzania inahitaji Bima ya Afya kwa wote na usawa wa matibabu kwa wote hivyo wao kama wanafunzi wamepokea muswaada huu kwa mikono miwili na kuwa sasa wanafunzi wataendelea kuunga mkono hatua hii.
Naye Bi. Jackline Tarimo kutoka Wizara ya Afya asema kuwa Serikali imedhamiria kuendelea kutoa huduma bora za afya nchini ambapo kwa sasa imeweza kuwa na vituo vya afya zaidi ya 10,000 hivyo kinachofanyika hivi sasa ni namna bora ya wananchi kwenda kupata huduma hizo bila kikwazo cha fedha kupitia utaratibu wa bima ya afya kwa wote

