Na Gideon Gregory, Dodoma.
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Masha J. Mshomba amesema kuwa katika nusu ya mwaka wa fedha iliyoishia Desemba 2022, Mfuko umekusanya shilingi bilioni 165.7 kutokana na mapato ya uwekezaji na vitega uchumi vya Mfuko.
Mshomba amebainisha hayo leo Februari 8,2023 Jijini Dodoma katika mkutano na waandishi wa habari wakati akielezea utekelezaji wa majukumu ya Mfuko huo katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Amesema kiasi hicho cha mapato hakijajumuisha ongezeko la thamani ya vitega uchumi vya Mfuko huo na kuongeza kuwa katika kipindi husika thamani ya vitega uchumi vya Mfuko (investment portfolio) ilikua na kufikia shilingi trilioni 5.8 ikiwa ni ongezeko la asilimia 7 ikilinganishwa na thamani ya shilingi trilioni 5.4 iliyofikiwa katika mwaka wa fedha ulioishia mwezi Juni 2022.
“Katika mwaka wa fedha unaoishia Juni 2023, thamani ya vitega uchumi vya Mfuko (investment portfolio) inatarajiwa kukua na kufikia shilingi trilioni 6.3 ambalo ni ongezeko la asilimia 17 ukilinganisha na thamani ya shilingi trilioni 5.4 iliyofikiwa mwezi Juni 2022,”amesema Mshomba.
Aidha, ameongeza kuwa kwa upande wa Uwekezaji, NSSF wana fursa za nyumba za makazi salama kupitia mfuko huo mwananchi anaweza kumiliki nyumba ya ndoto yake kwa kulipa gharama ya nyumba kwa mkupuo mmoja au kulipa kidogo kidogo wakati wakiendelea kuishi katika nyumba husika na nyumba hizo zipo Dungu, Mtoni Kijichi na Toangoma mjini Dar es Salaam.
Sanjari na hayo, amesema serikali imetekeleza mikakakati mbalimbali ya kuvutia wawekezaji wakubwa ikiwa ni pamoja na kupitia maonesho ya filamu ya The Royal Tour.
“Mikakati hiyo imekuwa na mchango mkubwa katika kuhakikisha kuwa miradi mikubwa ya kimkakati kama vile ujenzi wa bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere, Nyanzaga Goldmine, Kiwanda cha mbolea Intracom, Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Msalato, Mgodi wa Uchimbaji wa Madini ya Nikeli (Tembo) uliopo Ngara, Daraja la Kigongo-Busisi Mwanza, kiwanda cha Sukari cha Bagamoyo, mradi wa umeme wa Rusumo na mradi wa reli ya kisasa ya SGR inakamilika,”amesema.
Amesema miradi hiyo pekee imechangia takribani wanachama wapya 33,066 na kwa ujumla mkakati huo wa Serikali umechangia katika ongezeko la wanachama na michango inayokusanywa na Mfuko.
Kutokana na juhudi mbalimbali za Serikali kuvutia uwekezaji na kufungua fursa mpya za biashara, wastani wa makusanyo ya michango kwa mwezi imeongezeka na kufikia shilingi bilioni 134 kutoka wastani wa shilingi bilioni 118 kwa mwezi katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 2022 ikiwa ni sawa na asilimia 14.


