STAKABADHI GHALA YABADILISHA MWENENDO WA BEI YA ZAO LA KOROSHO.

MUUNGANO   MEDIA
0

Na Gideon Gregory, Dodoma.

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB), Asangye Bangu amesema kuwa baada ya mfumo wa Skabadhi Ghala kuanzishwa mwenendo wa bei ya zao la Korosho na uzalishaji umebadilika ghafla na kuanza kuwa na matokeo chanya (positive trend). 

Bangu ameyasema hayo wakati akiongea na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Bodi hiyo katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita leo Februari 15, 2023 kwenye ukumbi wa Idara ya Habari-MAELEZO jijini Dodoma.

Amesema baada ya kuanzishwa kwa mfumo huo palikuwa na ongezeko la asilimia 164% la bei kutoka Ths 350.00 msimu wa 2006/07 hadi kufikia Tsh 925.00 msimu wa 2007/08 mwaka wa kwanza wa Mfumo katika miaka minane tokea kuanzishwa kwa Mfumo 2007/08 hadi 2014/15 wastani wa ongezeko la bei kwa mwaka ulikuwa 25% kulinganisha na ongezeko la bei kabla ya  kuanzishwa kwa Mfumo la 12% kwa mwaka kuanzia mwaka 1998/99 hadi 2006/07.

“Kwa upande wa uzalishaji, tokea kuanzishwa kwa Mfumo 2007/08 hadi 2020/21 ukuaji wa uzalishaji umekuwa ukiongezeka kwa wastani wa 12% kwa mwaka ikilinganishwa na ukuaji wa 2% kwa mwaka kabla ya kuanzishwa kwa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala,”amesema.

Aidha, ameongeza kuwa mwaka 2021, Bodi hiyo iliwezesha kuanza kutumika kwa Mfumo huo mkoani Songwe katika zao la Ufuta na Morogoro katika zao la Kakao licha ya upinzani mkubwa uliokuwa ukiletwa na wanufaika wa mifumo holela katika maeneo hayo. 

“Mkoa wa Songwe wakulima walifanikiwa kukusanya tani 348.850 zilizowaingizia thamani ya Shilingi Milion 772.8 na kuwapa wastani wa bei ya Shilingi 2,221.53 ambayo ilikuwa ya juu kuliko iliyopatikana kwa wakulima waliouza nje ya Mfumo ambayo ilikuwa na wastani wa Tsh 1,200.00 hadi 1,700.00 pekee,”amesema. 

Stakabadhi ya Ghala ni hati maalumu inayotolewa na Meneja dhamana kwa mweka mali katika Ghala Kuu inayotaja umiliki, idadi na sifa za ubora wa mali iliyowekwa ghalani na hati hiyo kwa mujibu wa sheria huchapwa na kutolewa na bodi ya Usiamizi wa Stakabadhi za Ghala pekee.

Ikumbukwe kuwa bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) ni taasisi iliyo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara iliyoundwa kwa Sheria namba 10 ya 2005 na Marekebisho Kifungu 4 Sura 339 R.E. 2016 iliyopewa majukumu chini ya Kifungu 5 (a-j) ikiwemo kutoa leseni kwa waendesha ghala, meneja dhamana na wagakuzi wa ghala kuchapa na kuidhinisha vitabu vya Stakabadhi za Ghala, kusajili na kuingiza taarifa za wadau muhimu wa mfumo, kuwakilisha nchi katika masuala ya taifa na kimataifa yahusuyo Mfumo wa Stakabadhi za Ghala pamoja na majukumu mengine kama taasisi.

Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)