NAIBU WAZIRI MAVUNDE AWATAKA WADAU WA KILIMO KUZINGATIA MIPANGO YAO KWA VIJANA IENDANE NA PROGRAMU YA BBT

MUUNGANO   MEDIA
0

 


Naibu Waziri wa Kilimo, *Mheshimiwa Anthony Mavunde* amewataka wadau wote wa maendeleo ambao wanatekeleza miradi mbalimbali yenye lengo la kuvutia na kuinua vijana katika sekta ya kilimo kufuata muelekeo wa Programu ya Jenga Kesho iliyo Bora (Building a Better Tommorow - BBT) ili kuongeza wigo mpana ziaidi wa kuwafikia vijana wengi.

Wito huo umetolewa leo tarehe 11 Februari, 2023 Jijini Iringa Naibu Waziri Mavunde aliposhiriki katika uzinduzi wa Mradi wa kuwawezesha Vijana na Wanawake katika mnyororo wa thamani wa kilimo awamu ya pili (*Generation Food Accelerator II)* chini ya ufadhili wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya kupitia mradi wa Agri-connect.

"Ni dhahiri kwamba ninyi wadau, mkishirikiana na Serikali katika kutekeleza miradi yenu, kutaleta tija kubwa zaidi kutokana na kwamba, kutazuia upelekaji wa rasilimaji fedha katika eneo hilo hilo moja kwa Serikali na Wadau wa sekta binafsi.

Changamoto zinazowakabili vijana katika kilimo zinafahamika zikiwemo ukosefu wa ardhi, mitaji, pembejeo, miundombinu ya umwagiliaji na uhifadhi na masoko ya uhakika ya mazao watakayozalisha.

Serikali ya Awamu ya Sita chini ya utashi wa kisiasa na mkazo mkubwa kwenye kilimo aliyouweka *Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan* inakwenda kutatua changamoto hizo kupitia programu ya vijana ya __*Building a Better Tommorow *__kwa kuwatafutia ardhi na kuwamilikisha, kujenga miundombinu ya umwagiliaji na uhifadhi, kuwapatia pembejeo, kuwapa mitaji na kuwaunganisha na masoko ya uhakika.

Tunataka na ninyi wadau wote wa maendeleo ya masuala ya vijana kuhakikisha kwamba katika utekelezaji wa programu zenu mbalimbali mnazingatia mipango na muelekeo wa serikali katika kuwahudumia vijana kwenye sekta ya kilimo.

Nimefurahishwa na namna ambavyo mradi huo umepangwa kutekelezwa ambapo kiasi kikubwa cha fedha kitaelekezwa katika kuwapa vijana mitaji na ujenzi wa miundombinu, hali aliyoeleza kuwa uendelevu mkubwa kwa kijana hata pale ambapo mradi utafika mwisho”Alisema Mavunde.

Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)