Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amewaelekeza viongozi na watendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela na Nyamagana mkoani Mwanza kusimamia ukamilishaji wa miradi ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ya afya na elimu ili itoe michango katika maendeleo ya taifa.
Mhe. Jenista ametoa maelekezo hayo kwa nyakati tofauti katika Wilaya ya Ilemela na Nyamagana wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF mkoani Mwanza.
Mhe. Jenista amesema hukuna sababu ya kusuasua katika ukamilishaji wa miradi hiyo ya afya na elimu kwa kuwa ni miradi muhimu sana na ikizingatiwa kuwa fedha yote ya ujenzi wa miradi hiyo ilishatengwa na kutolewa na Serikali ya Awamu ya Sita.
Mhe. Jenista amesisitiza usimamizi mzuri wa miradi hiyo ya afya na elimu ambayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia TASAF ametoa fedha nyingi ili iwanufaishe walengwa na kuboresha utoaji wa huduma katika sekta hizo muhimu kwa jamii.
Mhe. Jenista amesema miradi yote ya elimu inayotekelezwa na TASAF itasaidia sana kuandaa rasilimaliwatu itakayoendeleza kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita ya kuleta maendeleo chanya kwa wananchi na taifa kwa ujumla.
“Shule hizi zinazojengwa kama zitatoa elimu bora kwa wanafunzi na wakapata ufaulu mzuri, nina hakika watakuwa ndio madaktari, walimu, wahandisi, wabunge, wakuu wa wilaya na viongozi wa vyama vya siasa wajao na kuongeza kuwa TASAF inandaa rasilimaliwatu ya kesho itakayokuwa na tija kwa maendeleo ya taifa,” Mhe. Jenista amesisitiza.
Akizungumzia faida ya miradi ya afya inayotekelezwa na TASAF, Mhe. Jenista amesema miradi hiyo ikikamilika itatoa huduma bora za afya kwa watumishi wa umma na wananchi ili waweze kuwa na afya bora inayowawezesha kushiriki shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii zitakazowawezesha kutoa mchango katika maendeleo ya taifa.
“Tukiwa na afya njema, tutashiriki vizuri shughuli mbalimbali za kiuchumi na hatimaye


