Na Emmanuel Kawau.
Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imesitisha leseni za usafirishaji abiria kwa mabasi 22 kwa kipindi cha mwezi Januari hadi February, 2023 kutokana na kuingilia mfumo wa kufuatilia mwenendo wa magari (VTS).
Akizungumza na waandishi wa habari Mkurugenzi udhibiti usafiri wa barabarani Johansen kahatano amesema vitendo vya kuingilia mfumo wa (VTS) husababisha mfumo kutotuma taarifa ama kutuma taarifa kwa kurukaruka (skipping).
"Hapa kuna baadhi ya mabasi ambayo baada ya wataalamu wa Mamlaka kufanya uchunguzi, waligundua betri za vifaa vya kufuatilia mwenendo wa mabasi (VTDs) zimeharibiwa na mfumo wa umeme kubadilishwa". Amesema Johansen.
Aidha amebainisha kuwa Kitendo cha kuingilia Mfumo wa VTS ni ukiukwaji wa Kanuni ya 51 ya Kanuni za Leseni za Usafirishaji kwa Magari ya Abiria za Mwaka 2020. Hivyo, Mamlaka imechukua hatua ya kusitisha leseni hizo kwa mujibu wa Sheria ya LATRA ya Mwaka 2019 na Kanuni zake za mwaka 2020.
"Kabla ya kurejeshewa leseni zao, watoa huduma wa mabasi husika walitakiwa kuwafikisha Jeshi la Polisi madereva wa mabasi husika ili wachukuliwe hatua kwa mujibu wa Sheria ya Usalama Barabarani Sura ya 168".
Kadhalika Mamlaka imewaandikia barua watoa huduma ambao vifaa vya kufuatilia mwenendo wa magari yao (VTDs) vinaonyesha viasharia vya kuchezewa na kuwataka watoe maelezo ya kwanini leseni zao zisisitishwe kutokana na kasoro hizo. Uchunguzi wa magari hayo bado unaendelea na pale itakapothibitika kuwa kuna uvunjaji wa kanuni leseni za magari husika zitasitishwa.
Mamlaka inawatahadharisha wamiliki wa mabasi na madereva wao kuzingatia Kanuni za Leseni za Usafirishaji (mabasi ya abiria) za Mwaka 2020 na Sheria ya Usalama Barabarani Sura ya 168 kwa kuongeza usimamizi wa huduma.
Pia Mamlaka inawaagiza wamiliki wote wa magari yanayotoa huduma kibiashara kuhakikisha madereva wao wote wamesajiliwa ifikapo tarehe 30 Aprili, 2023. Usajili unafanyika kwenye ofisi zote za LATRA Tanzania Bara na hivyo madereva wote waelekezwe kufika kwenye ofisi za LATRA ili waweze kusajiliwa.
"Mamlaka imeendelea kutekeleza jukumu la usajili wa madereva wa vyombo vya moto kibiashara kwa mujibu wa kifungu Na 5(1)(e) cha Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini Sura ya 413. Jumla ya madereva 13,291 wameshasajiliwa kwenye mfumo wetu na kati yao madereva 904 wameshafanya mitiahani kwa ajili ya kuthibitishwa" Amesema kahatano.
Kwa madereva watakaoshindwa kufika kwenye ofisi za LATRA wanaweza kutuma maombi ya kusajiliwa kupitia anuani ya https://rrims.latra.go.tz/login. Maombi ya kusajiliwa yaambatishwe Leseni ya udereva, Cheti cha taaluma ya udereva kutoka Chuo kinachotambulika na Serikali na Taarifa ya Uthibitisho wa afya kutoka Hospitali ya Serikali. Fomu ya Uthibitisho wa Afya inapatikana kwenye tovuti www.latra.go.tz na ofisi za LATRA.


