Katika kulinda usalama wa bahari kuu Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu imesema kuwa wameweka mifumo ya kulinda usalama ikiwa ni pamoja na kutumia mifumo ya kufuatilia meli ndani ya maji na kutumia doria za ndege kwa ajili ya kuangalia kinachofanyika.
Hayo yameelezwa leo Februari 8 ,2023 Jijini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Dkt.Emmanuel Sweke katika kikao na waandishi wa habari kuhusu Maendeleo ya mamlaka hiyo toka imeanzishwa mwaka 2010.
“Mamlaka hii katika kipindi cha mwaka 2022 hadi kufikia wiki mbili zilizopita uvuvi wa bahari kuu umeliingizia pato la taifa kiasi cha sh.bilioni 4.1 kwa shughuli za utoaji wa leseni kwa meli za uvuvi,”amesema.
Amesema pamoja na Uvuvi kuwa ni gharama kubwa lakini umeweza kuliingizia pato taifa kwa njia za utoaji leseni kwa meli za ndani na nje ambazo zinataka kufanya biashara ya uvuvi katika bahari kuu.
Dkt Sweke ameongeza kuwa uvuvi wa bahari kuu umekuwa na majukumu mbalimbali ikiwa ni pamoja na utoaji wa leseni kwa meli ambazo zinatakiwa kufanya uvuvi na kuhakikisha zinapokuwa zimepewa leseni zinakuwa na bendera ya Tanzania.
Sambamba na hayo, amezungumzia suala la maendeleo ya mapato ndani ya bahari kuu ambapo amesema tayari mwekezaji kutoka nchini Uhispania anatarajia kujenga kiwanda cha kuchakata samaki ambacho kitajengwa katika bandari ya Tanga .
“Mpaka kiwanda hiki kikamilike kitagharimu kiasi cha dola za Marekani milioni 10, ambapo kitazalisha ajira kwa watanzania 100 na kitakuwa kinahakata takribani tani 200 kwa siku,”amesema.
Aidha, ameeleza kuwa bado mamlaka inakabiliwa na changamoto ya ajira ya moja kwa moja hivyo wapo katika mchakato wa kuanza kutao ajira kwa maafisa na waangalizi.
