eGA KUFIKISHA MTANDAO WA MAWASILIANO SERIKALINI KATIKA WILAYA ZOTE NCHINI.

MUUNGANO   MEDIA
0

Na Gideon Gregory, Dodoma.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), Mhandisi Benedict Ndomba amesema mamlaka hiyo imepanga kupanua uwezo wa Mtandao wa Mawasiliano Serikalini (Government Network) na kuufikisha katika Wilaya zote nchini ili kurahisisha utekelezaji wa jitihada za serikali mtandao na kuwafikishia huduma wananchi wote popote walipo. 

Mhandisi Ndomba ameyabainisha hayo leo Februari 23,2023 Jijini Dodoma, Wakati akiongea na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka hiyo katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Amesema mpango mwingine ni Kupitia na kutathmini hali ya usalama wa Mifumo na miundombinu ya Serikali Mtandao na kuzishauri Taasisi za Umma katika maeneo ya kuboresha, pamoja na kufuatilia utekelezaji wake ili kuhakikisha kuwa Mifumo na Miundombinu ya TEHAMA inafanya kazi wakati wote kwa ufanisi na usalama.

“Mamlaka kwa kushirikiana na Taasisi mbalimbali za Umma, imefanikiwa kutengeneza mifumo mbalimbali ya kisekta inayotumika katika taasisi hizo, ikiwemo

mfumo wa ukusanyaji wa Malipo ya Serikali Kielektroniki (GePG) ambao umetengenezwa na Mamlaka kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango, mfumo huu unaimarisha uwazi na udhibiti katika ukusanyaji mapato ya Serikali,”amesema. 

Aidha ameongeza kuwa mpaka sasa kuna tasisi na vituo vya kutolea huduma 948 zinatumia Mfumo huu.

Akizungumzia mipango yao kwa miaka 10 ijayo amesema katika kuhakikisha wanaijenga Serikali ya Kidijiti, eGA itaandaa na kutekeleza mikakati madhubuti ili kuimarisha zaidi utekelezaji wa jitihada za Serikali.

“Mamlaka itaandaa uwezo wa kutumia teknolojia mpya zinazoibuka, hasa zile za akili bandia, sarafu za kidijiti na teknolojia za kifedha, ili kuwezesha maboresho ya kiutendaji katika Taasisi za Umma na utoaji wa huduma kwa umma,”amesema.

Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) ni taasisi ya Umma iliyoanzishwa kwa Sheria ya Serikali

Mtandao Na. 10 ya mwaka 2019, ikiwa na majukumu ya kuratibu, kusimamia na kukuza jitihada za Serikali Mtandao, pamoja na kusimamia uzingatiaji wa Sera, Sheria, Kanuni, viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao katika Taasisi za Umma.

Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)