Serikali kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) inatarajia kuanza utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji wa Rufiji utakaohudumia mikoa ya Dar es salaam na Pwani.
Mradi utazalisha lita milioni 750 kwa siku, ni moja ya manufaa makubwa kwani utawezesha maji ya Mto Rufiji kuweza kutumika kuzalishia maji kwa ajili ya mikoa hii miwili ya biashara na viwanda.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya DAWASA Jenerali Mstaafu Davis Mwamunyange amesema wakati wa ziara ya Bodi iliyolenga kukagua chanzo cha mradi wa kufua umeme cha Mwalimu Julius Nyerere (JNHPP).
“Tumefurahishwa sana na utekelezaji wa mradi huu na tunaipongeza sana Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, kwa kusimamia ukamilishaji wa mradi huu utakaoleta tija kubwa kwa Taifa. Kasi ya ukamilishaji wa mradi huu ni kubwa, na nipende kusema kuwa kupitia mradi huu DAWASA itaenda kutekeleza mradi wa maji Rufiji utakaohudumia mkoa wa Pwani na sehemu ya Mkoa wa Dar es salaam.” Alisema
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema kuwa utekelezaji wa mradi wa maji Rufiji utaenda kuongeza na kuimarisha kiwango cha upatikanaji wa maji katika eneo la kihuduma la DAWASA.
“Ziara hii ya Bodi ya Wakurugenzi imekuja kuona chanzo cha maji cha mradi wa Rufiji ambao ni bwawa la Mwalimu Nyerere ambao upo katika hatua za mwisho za utekelezaji wake. Kwa sasa Mamlaka inazalisha lita Milioni 590 wakati mahitaji yakiwa lita Milioni 540. Kupitia mradi wa maji Rufiji tunategemea kuzalisha Lita milioni 750 zitakazosaidia kuimarisha upatikanaji wa huduma kwa Mkoa wa Pwani pamoja na Wilaya jirani alifafanua Mhandisi Luhemeja.
“Utekelezaji wa mradi wa maji Rufiji upo katika hatua ya kufanya usanifu na kuandaa michoro ya mradi baada ya kukamilisha upembuzi yakinifu" Luhemeja amesema.
Mtambo wa uzalishaji maji Rufiji unatarajiwa kujengws katika kijiji cha Mloka Wilayani Rufiji. Kijiji hicho kipo baada ya mradi wa JNHPP.


