𝗛𝗔𝗟𝗠𝗔𝗦𝗛𝗔𝗨𝗥𝗜 𝗭𝗔𝗛𝗔𝗠𝗔𝗦𝗜𝗦𝗛𝗪𝗔 𝗞𝗨𝗧𝗘𝗡𝗚𝗔 𝗠𝗔𝗘𝗡𝗘𝗢 𝗬𝗔 𝗕𝗕𝗧.

MUUNGANO   MEDIA
0

 


Halmashauri za Wilaya nchini zinahamasishwa kuendelea kutenga maeneo kwa ajili ya  mashamba ya pamoja(Block Farm) kwa ajili ya kuwezesha Vijana kufanya kilimo biashara kupitia Programu ya Building a Better Tomorrow (BBT)

Wito huo umetolewa na Mhandisi Godwin Makori ambaye anaratibu na kusimamia kazi kuhakiki mashamba  na kupima mashamba kwa ajili ya kuyaandalia hati miliki na kupima afya ya udongo katika maeneo ambayo hali za afya ya udongo hazijulikani.

Kazi hiyo inajumuisha wataalam kutoka Wizara ya Kilimo, Sekretarieti ya Mkoa, Kamishna wa Ardhi Msaidizi, Halmashauri za Wilaya na Serikali za  Vijiji katika mkoa wa Kagera.

Akiwa katika kijiji cha Minazi kata ya Bujugo Halmashauri ya Bukuba Vijijini Mhandisi Makori amesema timu ya wataalam itayafikia maeneo  yaliyotengwa na Halmashauri na kuyapima ili kuwezesha upatikanaji wa Hati miliki na kupima afya ya udongo ili vijana watakapoanza kuzalisha katika  mashamba hayo wazalishe kwa uhakika kwa kuwa watakuwa wanajua mazao yanayofaa kulimwa na kulingana hali  ya udongo.

Kwa upande wake  Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Bw. Toba Nguvila amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa hatua ya kuwezasha vijana kupitia BBT kwani uzalishaji wa mazao utaongezeka na vijana wa Tanzania watapata ajira.

Ameongeza kuwa Viongozi na wananchi wa mkoa wa Kagera  wanaunga mkono jitihada za  Wizara ya Kilimo chini ya uongozi wa Waziri wa Kilimo Mhe.Hussein Bashe  kwa maslahi mapana ya maendeleo ya mkoa wa Kagera na Taifa kwa ujumla.

Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)