KUVAMIWA NA FISI NA UKOSEFU WA UMEME ZAGEUZWA FURSA SHULE YA MSINGI MWANHEGELE ILIYOONGOZA SHULE ZA MSINGI ZA SERIKALI TANZANIA.

0


 Mwonekano kwa mbele shule ya Msingi Mwanhegele Wilayani Maswa Mkoani Simiyu.


Moja ya kombe lililotolewa na serikali kwa shule ya Msingi Mwanhegele kutokana na shule hiyo kuendelea kufanya vizuri mitihani ya Taifa.



Mmoja wa walimu katika shule ya msingi Mwanhegele akitekeleza majukumu yake ya ufundishaji


Mazao ya chakula yanayotumika katika kipindi cha makambi ya masomo.


Na.Faustine Gimu Galafoni,Maswa Simiyu.

 

Shule ya Msingi Mwanhegele iliyopo Wilayani Maswa Mkoani Simiyu ambayo imekuwa ikishika kumi bora kwa miaka 6 mfululizo katika shule za serikali Tanzania huku  matokeo ya mwaka jana ikishika nafasi ya Kwanza  kwa shule za serikali  ambapo changamoto zinazoikabili shule hii ikiwemo kukumbwa na wanyama wakali kama vile fisi na ukosefu wa umeme  zimegeuzwa kama fursa.

 

  Mwalimu mkuu wa shule ya Msingi Mwanhegele  ,Mashala Kija  akifanya mahojiano maalum na Mtandao huu  mwanzoni mwa Juma lililopita  alisema moja ya juhudi wanazozifanya ni kuanzisha makambi ya kujisomea nyakati zote za usiku na  mchana kwa madarasa  yanayokabiliwa na mitihani ya kitaifa ambapo mwaka jana palitokea changamoto ya kuvamiwa na wanyama wakali  wakiwemo fisi  lakini walishirikiana na wananchi kuwasaka fisi na kuendelea kujisomea nyakati za usiku.

“Shule hii imefanya jitihada mbalimbali ambapo mwaka jana imekuwa ya Kwanza Tanzania,changamoto kubwa zinazoikabili shule hii mfano,wakati tukiwa makambi tulianza kuvamiwa na fisi katika maeneo haya lakini tuliweza kupambana kwa kushirikiana na wananchi ,hatukurudi nyuma maana nyakati za usiku wanafunzi wakiwa wajisomea fisi walikuwa wanakuja hii ni kutokana na jiogerafia ya maeneo haya”alisema mwalimu Mashala.

Aidha,Mwalimu mkuu huyo alisema changamoto ya kutokuwa na miundombinu ya umeme shuleni hapo imewapa fursa ya kununua umeme jua[sola]kwa ajili ya kuruhusu wanafunzi kujisomea nyakati za usiku

“Licha ya shule hii kufanya vizuri tunakabiliwa na changamoto ya kutokuwa na umeme ,na umeme tunaotumia hadi sasa ni umeme wa jua hii ni kutokana na wazazi kushirikiana kwa kufanya michango na kufanikisha kununua umeme jua[sola] lakini mkakati wa serikali ni kutandaza umeme wa TANESCO kwa mujibu wao walisema umeme huo unaweza kuwasha kuanzia mwezi wanne”alisema.

Mwalimu Mashala aliainisha Changamoto nyingine ni utokuwa na miundombinu ya nyumba za walimu hata moja hali ambayo huwalazimu walimu kupanga wilaya jirani ya Kwimba mkoani Mwanza.

“Kwa kweli hii ni changamoto kubwa kwani walimu  wanapanga wilaya jirani ya Kwimba mkoani Mwanza ,na wanapofundisha usiku wakimaliza inabidi wasubiriane kwenda nyumbani nyakati za usiku kwani ni mbali kidogo  hilo ndio ombi letu kubwa kwa serikali itusaidie angalau hata nyumba mbili za kuanzia maana hakuna hata nyumba moja ya mwalimu”alifafanua Mwalimu Mashala.

Mwenyekti wa Kamati ya Shule ya Msingi Mwanhegele ,Mathias Gabriel alisema ushirikiano kati ya kamati ya shule na walimu ndio nguzo muhimu inayosaidia kufaulisha wanafunzi .

Sisi kama kamati ya Shule tuna ushirikiano mkubwa na walimu na tunawaheshimu sana kutokana na kazi ngumu wanazofanya na huwa tunajitahidi kuwatia moyo”alisema .

 

 

 

Baadhi ya walimu katika shule hiyo   walisema  umoja na ushirikiano  ndio nguzo muhimu inavyochochea kiwango cha ufaulu katika shule hiyo.

“moja ya mkakati tunaofanya ni kuhakikisha mtoto apandi darasa kama hajui kusoma ,kuandika na kuhesabu hivyo ushirikiano wetu pamoja na uongozi na kamati ya elimu umekuwa nguzo muhimu na tunahakikisha tunakuwa lugha moja”alisema mmoja wa walimu hao.

Kwa upande wao baadhi ya wanafunzi darasa la saba shule ya Msingi Mwanhegele  akiwemo  Agnes Paul Cosmas pamoja  Elia Andrea  waliahidi kufanya vizuri kwa mwaka huu kama walivyofanya watangulizi wao.

 

Katika utatuzi wa changamoto za ukosefu wa miundombinu shuleni hapo,Afisa Elimu,Wilaya ya Maswa Lucy Kulong’wa alisema serikali ina mpango wa ujenzi wa nyumba za walimu katika shule mbalimbali wilayani Maswa.

 

Ikumbukwe kuwa shule ya msingi Mwanhegele Maswa Simiyu imekuwa ya kwanza  kwa shule za serikali katika matokeo ya mtihani kumaliza elimu ya Msingi Tanzania  zikifuatiwa na shule ya Msingi Kagera ,shule ya msingi Stesheni Lindi,shule ya msingi Butimba B,Butimba ,Majengo mkoani Lindi ,Mnarani Mkoani Mwanza ,Kisimani Mkoani Arusha,Nyasa mkoani Mbeya na nafasi ya kumi ilikuwa ni shule ya Msingi Mianzini kutoka mkoani Lindi.

MWISHO.

Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)