o
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka mawaziri, naibu mawaziri, makatibu
wakuu, wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi kujenga utamaduni wa kutoa
taarifa za fedha za miradi ya maendeleo kwa wananchi badala ya kusubiri
kufanya hivyo katika ziara za viongozi wakuu.
Majaliwa
ametoa agizo hilo jana Jumamosi Januari 6, wakati akizungumza na
watumishi na madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Nyasa kwenye kikao
kilichofanyika mjini Mbamba Bay, wilayani Nyasa mkoani Ruvuma.
“Kuanzia
sasa ninaagiza, viongozi wote wa ngazi za juu wakiwemo mawaziri hadi
wakurugenzi na hata ninyi wakuu wa idara mnawajibika kutoa taarifa za
fedha tunazopeleka kwenye miradi kwa sababu wananchi wana haki ya kujua
utekelezaji wa ahadi za Serikali,” amesema.
Amewataka
kila wanapoenda kwenye ziara ya kikazi vijijini, waelezee thamani za
kazi zilizofanyika na waeleze ni lini miradi hiyo itakamilika.
“Mnapopata fursa ya kupanda jukwaani, tumieni wasaa huo kueleza kazi kubwa ambazo zimefanywa na Serikali,” amesema na kuongeza,
“Elezeni
Serikali imeleta fedha kiasi gani, kwa ajili ya kitu gani na kwa
kufanya hivyo, mtasaidia kutoa taarifa za utekelezaji wa ahadi
zilizotolewa na Rais John Magufuli wakati wa kampeni.”
Amesema
wananchi wana haki ya kupatiwa taarifa za utendaji wa Serikali yao na
akawataka viongozi hao wasisubiri ziara za viongozi wa kitaifa.
“Nendeni mkaongee na wananchi, msiwaachie wakuu wa wilaya au wabunge peke yao ndiyo waseme na wananchi,” amesema.