Chama
cha ACT-Wazalendo kimetangaza mikakati minne ya kipaumbele
itakayoitumia kufanya siasa mwaka huu, ikiwemo kuimarisha ushirikiano na
vyama vya wafanyakazi.
Akizungumza
leo Jumapili, Januari 7, 2018, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mawasiliano
ya Umma ya chama hicho, Ado Shaibu amesema wanatambua kwamba
wafanyakazi wanakabiliana na changamoto mbalimbali.
Amesema
chama hicho kitawasemea wafanyakazi wanaolipwa mishahara duni,
mazingira duni ya kufanyia kazi na uonevu unaofanywa na waajiri.
Shaibu
amesema jambo jingine litakalofanywa mwaka huu ni kuimarisha
ushirikiano na vyama vya siasa hasa katika kudai demokrasia na Katiba
Mpya.
“Tutaongeza
ushirikiano na vyama vingine vya upinzani katika kudai Katiba Mpya,
tunahitaji kushirikiano ili kufanikisha hili,” amesema.
Amesema mwaka huu chama hicho kitafanya uchaguzi wa ndani ya chama kuanzia ngazi ya shina hadi taifa.
“Demokrasia
inatakiwa ianzie ndani ya chama, tunawaomba wanachama wetu wajitokeze
kugombea nafasi mbalimbali za uongozi,” amesema.
Shaibu
amesema chama hicho kitaongeza juhudi katika kupambana na haki za
kijamii hasa katika kuwapigania wastaafu na bima ya afya kwa watu walio
nje ya mfumo rasmi wa ajira.
“Mwaka
2018 utakuwa wa kuimarisha ushirikiano wetu na wanyonge katika
kupigania haki za kijamii na kurejesha misingi ya utu na
heshima,”amesema.