Baraza la
madiwani la halmashauri ya Msalala Wilayani Kahama Mkoani Shinyanga limeiomba halmashauri
hiyo kuyawekea kipaumbele cha kwanza maboma yaliyokaa kwa muda mrefu bila kupauliwa
ili yaweze kukamilika hali itakayoondoa migogoro ya wananchi baina yao na wawakilishi
wao.
Wakizungumza
katika kikao cha kujadili bajeti kwa mwaka wa fedha 2018/2019 diwani wa kata ya
Mwalugulu Flora Sagasaga na diwani wa Kata ya Ikinda Matrida Musoma, wamesema
kuwa ni vyema bajeti ikajikita kusaidia kata zao kwanza kutokana na changamoto
zilizopo.
Akijibu
hoja hizo Kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya Msalala ambaye pia ni mhasibu wa
halmashauri hiyo Masatu Mnyoro amesema kuwa wananchi hawana budi kuendelea kuwa
na uvumilivu.
Kwa upande
wake mbunge wa jimbo la Msalala Ezekiel Maige amesema ni vyema kushirikiana na
idara ya Afya kufanya tathmini ya maboma ya zahanati ili na mengine yakamilike
huku pia akitoa wito kwa halmashauri ya Msalala kuwa na mpango madhubuti ya
matumizi ya fedha.