Waziri
wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako amekataa kutoa usajili kwa Shule ya
Msingi Njalu iliyopo wilayani Itilima, Mkoa wa Simiyu kutokana na
kutokidhi vigezo.
Shule hiyo imejengwa na wananchi kwa kushirikiana na mbunge wa Itilima (CCM), Njalu Silanga.
Akizungumza
katika mkutano uliofanyika jana katika shule hiyo iliyopewa jina la
Njalu kutokana na mchango wa mbunge huyo katika ujenzi, Profesa
Ndalichako alisema shule hiyo haijakidhi vigezo vya usajili.
Mbele
ya wakazi wa Kijiji cha Habiya ilipo shule hiyo, waziri Ndalichako
alikataa ombi la mbunge huyo kuisajili na kuagiza upungufu uliopo
urekebishwe kwanza kabla ya wizara kuisajili shule hiyo ya umma.
Miongoni mwa upungufu huo ni kuwa na vyumba vitano pekee vya madarasa badala ya vinane vinavyohitajika.
Mengine
ni matundu ya vyoo, ambayo kati ya 10 yanayohitajika, yapo matano
pekee, huku ikiwa na chumba kimoja cha ofisi ya walimu.
Profesa Ndalichako alisema wizara itatoa mifuko 100 ya saruji kusaidia kuondoa upungufu uliopo.
“Tumeona
kuna upungufu hatutaweza kutoa kibali cha kuisajili, badala yake
mkamilishe yanayohitajika kwa utaratibu wa kisheria wa kufungua shule.
Niwahakikishie kuwa, Wizara ya Elimu hatuna urasimu ni lazima tuwe
makini kwa kusimamia vigezo hivyo,” alisema Profesa Ndalichako.
Alisema
licha ya kuwapo kwa mahitaji ya shule katika eneo hilo ambalo lina
wanafunzi wapatao 633, ni lazima kuzingatia vigezo ambavyo vitakaguliwa
na wataalamu kutoka idara ya udhibiti ubora wa elimu na ofisi ya ofisa
elimu wilaya.
Awali,
Silanga alielekeza lawama kwa watumishi wa Serikali na hasa wa idara ya
elimu mkoani Simiyu kwa kushindwa kutumia utaalamu wao kuwaelimisha
wananchi kuhusu vigezo vinavyotakiwa kabla ya shule kusajiliwa.
“Timu
ya wataalamu ishuke itoe maelekezo. Majengo mengi yanavunjwa,
wasimamizi tunao lakini hawatekelezi majukumu yao hivyo watimize wajibu
wao kuliko kuwakatisha tamaa wananchi katika kuchangia shughuli za
maendeleo,” alisema.
Silanga
alimwomba Waziri Ndalichako kuwapatia usajili wakati wakiendelea
kushughulikia upungufu uliojitokeza kwa kipindi cha muda mfupi kabla ya
shule kufunguliwa Januari 8 mwakani ombi ambalo hata hivyo,
lilikataliwa.
Mkuu
wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka alisema hawawezi kuwaadhibu wananchi
na mbunge, hivyo ni lazima wahakikishe upungufu uliopo unaondolewa kabla
ya Januari 15 mwakani.
Katika
kuunga mkono jitihada hizo, Mtaka alitoa mifuko 50 ya saruji; huku mkuu
wa Wilaya ya Itilima, Benson Chilangi pia akitoa mifuko 50.
Halmashauri ya Wilaya ya Itilima imeahidi kutoa mabati na mbao zitakazohitajika katika ujenzi.