TDB YATOA MAFUNZO YA USINDIKAJI BORA WA MAZIWA NANENANE 2026

MUUNGANO   MEDIA
0

 

DODOMA.

Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB) imeendelea kutoa elimu na mafunzo ya usindikaji bora wa maziwa kwa wananchi na wadau mbalimbali wanaotembelea banda lake katika Maonesho ya Wakulima Nanenane 2026 yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. John Samwel Malecela, jijini Dodoma. 


Mafunzo hayo yaliyotolewa Agosti 6, 2026 yanalenga kuongeza uelewa kuhusu matumizi ya teknolojia sahihi katika usindikaji wa maziwa, kuongeza thamani ya bidhaa za maziwa na kuimarisha usalama wa chakula.


Akitoa mafunzo hayo, Afisa Mtekinolojia wa Chakula wa Bodi ya Maziwa Tanzania, Bw. Israel Mwingira, alieleza kuwa usindikaji wa maziwa kwa kuzingatia kanuni za usafi na ubora ni msingi wa kuzalisha bidhaa salama zinazokidhi viwango vya kitaifa na kimataifa.


Alisisitiza umuhimu wa kutumia teknolojia sahihi katika hatua zote za ukusanyaji, uhifadhi na usindikaji wa maziwa ili kupunguza upotevu, kuongeza muda wa kuhifadhi bidhaa na kuimarisha ushindani wa Tasnia ya Maziwa nchini.


Kwa upande wake, Meneja wa Kampuni ya PROMACO, Bw. Joachim Mbaruku, alitoa mafunzo kuhusu matumizi ya vimea vya maziwa (starter cultures) katika usindikaji wa maziwa mtindi. 


Alieleza kuwa matumizi sahihi ya vimea hivyo husaidia kuzalisha maziwa mtindi yenye ubora wa hali ya juu, ladha nzuri na yanayokidhi viwango vya usalama wa chakula. 


Aidha, aliwahamasisha wasindikaji na wajasiriamali kutumia teknolojia za kisasa ili kuongeza thamani ya maziwa na kupanua fursa za biashara katika soko la ndani na nje ya nchi.


Wananchi na wadau walioshiriki mafunzo hayo walieleza kuwa elimu waliyoipata itawasaidia kuboresha shughuli zao za usindikaji wa maziwa, kuongeza ubora wa bidhaa wanazozalisha na kuimarisha ushindani katika soko.



Kupitia mafunzo hayo, TDB inaendelea kutekeleza jukumu lake la kuendeleza Tasnia ya Maziwa nchini kwa kutoa elimu kwa wadau, kuhamasisha matumizi ya teknolojia za kisasa na kukuza uzalishaji wa maziwa salama na yenye ubora, sambamba na kuongeza mchango wa Tasnia hiyo katika ukuaji wa uchumi na kuboresha lishe ya Watanzania.

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)