Na Avelina Musa - Dodoma.
Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) wameingia makubaliano ya ushirikiano yenye lengo la kuimarisha matumizi ya teknolojia katika uzalishaji, uchambuzi na usambazaji wa takwimu rasmi Nchini.
Makubaliano hayo yamesainiwa katika hafla iliyofanyika Jijini Dodoma, ambapo taasisi hizo zimeeleza dhamira ya kushirikiana katika kutumia maarifa ya kisayansi, ubunifu na teknolojia za kisasa ili kuongeza ufanisi na ubora wa takwimu zinazozalishwa nchini.
Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dkt.Amina Msengwa amesema Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inazalisha takwimu rasmi nchini kwa kutumia vyanzo mbalimbali, ikiwemo tafiti na sensa, kwa lengo la kuhakikisha Taifa linapata takwimu sahihi na zenye ubora kwa ajili ya kupanga na kufanya maamuzi.
"Tafiti na sensa ni miongoni mwa nyenzo muhimu zinazotumika katika kukusanya taarifa zinazozalisha takwimu rasmi na ushirikiano huu unalenga kuunganisha utaalamu wa NBS katika uzalishaji na uratibu wa takwimu rasmi na uwezo wa kitaaluma wa kiteknolojia uliopo UDSM na NM-AIST, hususan katika maeneo ya sayansi ya takwimu, sayansi ya data, akili unde (Artificial Intelligence), mifumo ya kidijitali na teknolojia za uchambuzi wa taarifa."amesema Dkt Amina.
Dkt.Amina amesema Ushirikiano wa NBS, UDSM na NM-AIST utachochea upatikanaji wa wataalamu wenye ujuzi unaohitajika katika eneo la sayansi ya data na teknolojia, pamoja na kuongeza matumizi ya tafiti na ubunifu katika kutatua changamoto zinazohusiana na uzalishaji wa takwimu nchini.
Aidha Mwenyekiti wa Bodi ya Usamamizi ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Mhe. Anne Semamba Makinda amesema ili Serikali iweze kupanga mipango itakayoweza kutatua changamoto zinazowakabili Wananchi, ni vema suala la matumizi ya teknolojia katika uzalishaji wa Takwimu rasmi nchini lizingatiwe na kutumiwa kikamilifu, badala ya Takwimu hizo kubaki kwenye machapisho bila kutumika ipasavyo.
Kwa Upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. William-Andey Lazaro Anangisye amesema ushirikiano huo unaakisi utekelezaji wa Dira 2050 ambayo inasisitiza maendeleo ya rasilimali watu, sayansi, teknolojia, ubunifu na maarifa kwa ajili ya mageuzi ya kiuchumi Nchini.
Naye Makamu Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM - AIST) Prof. Maulilio John Kipanyula amesema maamuzi muhimu na makubwa nchini, hayawezi kujengwa kwa hisia au makisio, badala yake yanahitaji Takwimu rasmi zenye Ushahidi wa kisayansi. :
Kupitia makubaliano hayo,Taasisi hizo zinatarajiwa kushirikiana katika tafiti, ubunifu wa mifumo na zana za kiteknolojia, kujenga uwezo wa wataalamu pamoja na kubadilishana maarifa yatakayosaidia kukabiliana na mahitaji yanayobadilika ya uzalishaji wa takwimu katika zama za kidijitali.


.jpg)


