Serikali kupitia Wizara ya Afya, kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) na wadau mbalimbali, imeanza maandalizi ya Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano na Ushirikishwaji wa Jamii wakati wa Dharura na Majanga (RCCE) kupitia kikao kazi cha siku tatu kinachofanyika mkoani Morogoro.
Kikao hicho kinawakutanisha wataalamu kutoka Wizara, taasisi za Serikali na wadau wa maendeleo wakiwemo Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), Shirika la Afya Duniani (WHO), Plan International na Shirika la Msalaba Mwekundu Tanzania kwa lengo la kuandaa nyaraka zitakazoongoza mawasiliano na ushirikishwaji wa jamii kabla, wakati na baada ya dharura za afya ya umma na majanga.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma, Maxmillian Kwangu, amesema mkakati huo ni hatua muhimu katika kuimarisha utayari wa Tanzania wa kukabiliana na dharura za afya ya umma na majanga mbalimbali.
"Ninawakaribisha katika kikao kazi hiki cha siku tatu kinacholenga kuandaa Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano na Ushirikishwaji wa Jamii wakati wa Dharura na Majanga (RCCE), Mpango wa Utekelezaji wa RCCE, Mfumo wa Ufuatiliaji na Tathmini wa RCCE, pamoja na Mfumo wa Uhamasishaji wa Jamii na Itifaki ya Mawasiliano wakati wa dharura na majanga," amesema Kwangu.
Aidha, amewahimiza washiriki kushiriki kikamilifu katika mijadala, kutoa mawazo kwa uwazi na kuchangia uzoefu pamoja na utaalamu wao ili kuwezesha kuandaliwa kwa nyaraka zenye ubora wa hali ya juu, zinazozingatia viwango na miongozo ya kitaifa pamoja na mahitaji na vipaumbele vya Wizara ya Afya.
Kwa upande wake, Mratibu wa Ushirikishwaji wa Jamii na Mawasiliano wakati wa Dharura kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), Ofisi ya Dar es Salaam, Bi. Awet Araya, ameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa juhudi zinazoendelea kufanyika katika kuimarisha utayari wa taifa wa kukabiliana na dharura na majanga mbalimbali ya afya ya umma.
Amesema nyaraka zitakazoandaliwa kupitia kikao hicho zitaweka mfumo wa pamoja unaozingatia ushahidi na mbinu bora za kuongoza utekelezaji wa afua za RCCE kabla, wakati na baada ya kutokea kwa dharura za afya ya umma.
Kupitia nyaraka hizo, wadau wote watakuwa na mwongozo unaofanana katika kuwasiliana na jamii, kuhamasisha ushiriki wao na kujenga imani miongoni mwa wananchi wakati wa kukabiliana na milipuko ya magonjwa na dharura nyingine za kiafya.
Ingawa Tanzania haijawahi kukumbwa na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola, kuendelea kwa milipuko ya ugonjwa huo katika baadhi ya nchi jirani kunakumbusha kuwa magonjwa ya mlipuko hayana mipaka. Hivyo, ni muhimu kuendelea kujiandaa mapema ili kuhakikisha taifa lina uwezo wa kukabiliana kwa ufanisi endapo tishio la mlipuko wa ugonjwa huo au dharura nyingine za afya ya umma litatokea.
Mkakati huo unatarajiwa kuimarisha uratibu wa mawasiliano ya hatari na ushirikishwaji wa jamii nchini, kuhakikisha jamii zinapata taarifa sahihi kwa wakati na kushiriki kikamilifu katika hatua za kuzuia na kudhibiti dharura za afya ya umma na majanga.