TAKUKURU YABAINI MAPUNGUFU MIRADI YA BILIONI 156 DODOMA

MUUNGANO   MEDIA
0

‎      

‎Na Mwandishi wetu - DODOMA.


‎TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Dodoma imebaini mapungufu katika miradi 36 ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 156 baada ya kufanya ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za umma katika kipindi cha Januari hadi Machi mwaka 2026.

‎Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 29, 2026 jijini Dodoma, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa huo Christopher Myava amesema ukaguzi huo umefanyika ili kuhakikisha miradi ya maendeleo inazingatia mikataba na thamani halisi ya fedha zinazotolewa na Serikali.

‎Amesema mapungufu hayo yamebainika katika sekta mbalimbali zikiwemo elimu, afya, maji, makazi pamoja na ujenzi wa barabara ambapo baadhi ya miradi haijatekelezwa kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa.

‎Myava amesema miongoni mwa dosari zilizogundulika ni pamoja na kutokuzingatiwa kwa BOQ katika ujenzi wa madarasa na mabweni katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Kibaigwa.

‎Ameeleza kuwa baadhi ya venti za milango ya mabweni zimewekwa nyavu badala ya vioo, huku masinki katika vyoo vya mabweni yakikosekana tofauti na maelekezo yaliyopo kwenye ramani za ujenzi.

‎Aidha amesema TAKUKURU imeendelea kufanya uchambuzi wa mifumo na kutoa mapendekezo yaliyochangia kuboreshwa kwa ratiba za upatikanaji wa maji pamoja na kuanzishwa kwa njia mbalimbali za wananchi kuwasilisha kero zao kwa viongozi.

‎Katika kipindi hicho, TAKUKURU imefanikiwa kuwafikia wananchi zaidi ya 5,300 kupitia semina, mikutano ya hadhara na vipindi vya redio kwa lengo la kutoa elimu kuhusu mapambano dhidi ya rushwa.

‎Sambamba na hayo, taasisi hiyo imepokea malalamiko 168 ambapo 83 yanahusu vitendo vya rushwa huku kesi 13 zikiendelea mahakamani. TAKUKURU imewataka wananchi kuendelea kushirikiana nayo kwa kutoa taarifa sahihi za vitendo vya rushwa kwa wakati.

Mwisho.

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)