ONE ACRE FUND YAUNGA MKONO JUHUDI ZA SERIKALI KUIINUA MAISHA YA WAKULIMA.

MUUNGANO   MEDIA
0


 

Na Avelina Musa  - Dodoma.

Katika Harakati za kuunga mkono juhudi za Serikali za kuongeza tija katika uzalishaji wa zao la Korosho Kampuni ya One Acre Fund Tanzania na Bodi ya Korosho Tanzania wameingia makubaliano ya ushirikiano yanayolenga kuongeza tija katika uzalishaji na uongezaji wa thamani ya zao la korosho, hatua inayotarajiwa kuleta manufaa zaidi kwa wakulima.

Makubaliano hayo yamejikita katika kuboresha maisha ya wakulima wa korosho kwa kuwawezesha kupata maarifa na mbinu bora zaidi za uzalishaji, pamoja na kuimarisha fursa za masoko ili wakulima wanufaike zaidi na zao hilo.


Akielezea Umuhimu wa Makubaliano hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Kampuni ya One Acre Fund Tanzania, Amar Khalid  Hamad amesema kusainiwa kwa makubaliano hayo ni hatua muhimu kwa Kampuni  hiyo katika kuwafikia na kuwawezesha wakulima wa korosho ili 
kuongeza tija katika uzalishaji wa zao hilo.


Hamad amesema kupitia makubaliano hayo, wakulima watapata mafunzo ya ugani na mbinu bora za kufuatilia uzalishaji na kupata fursa zaidi za masoko zitakazowawezesha kunufaika zaidi na zao la korosho.

"Makubaliano haya yatasaidia  kuimarisha mnyororo wa thamani wa korosho, kuongeza kipato cha wakulima na kuboresha maisha ya familia na jamii zinazotegemea zao hili kiuchumi"amesema.

Awali Bi.Neema Basila ambaye ni Afisa Mwandamizi wa mahusiano na Serikali  kutoka One Acre Fund Tanzania amesema Kampuni hiyo inahudumia wakulima katika mikoa 7 nchini Tanzania.



"Amesema Mikoa hiyo ni Songwe,Iringa,Morogoro,Mtwara,Singida,Mbeya na Njombe ambapo kampuni imejikita katika Uingizaji na Usambazaji wa pembejeo za kilimo pamoja na mbegu za kisasa pamoja na huduna za Ugani"amesema Bi.Neema


Aidha,Kwa Upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania, Francis Alfred Mbaye, amesema ushirikiano huo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha sekta ya korosho na kuhakikisha wakulima wanaendelea kupata fursa zitakazowawezesha kuongeza uzalishaji na thamani ya mazao yao.

Mbaye ameipongeza Kampuni ya One Acre Fund Tanzania kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali katika kuhakikisha mkulima wa Korosho anazalisha kwa tija na kukuza sekta ya korosho Nchini.







Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)