Na Avelina Musa - DODOMA.
Mbunge wa Viti Maalum Mhe Cecilia Pareso(CCM) amepongeza juhudi za Serikali katika kuimarisha elimu ya ufundi na stadi za kazi kupitia ujenzi wa vyuo vya VETA Nchini.
Mhe.Paresso amesema hayo wakati akichangia mjadala wa bajeti ya Wizara ya Elimu bungeni Jijini Dodoma ambapo amesema Serikali ya Rais Dkt.Samia imefanya maboresho makubwa katika sekta ya elimu nchini yaliyolenga kuendana na mahitaji ya sasa.
Amesema maboresho hayo ya sera ya elimu ni sehemu ya mafanikio makubwa ya Serikali ya Rais Samia katika kuhakikisha mfumo wa elimu unakuwa jumuishi na wenye kutoa fursa sawa kwa wote
"Hatua ya kuruhusu wanafunzi waliopata ujauzito kurejea shuleni imefungua fursa kwa maelfu ya watoto wa kike kuendelea kutimiza ndoto zao za elimu baada ya awali kukatisha masomo kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo ndoa za utotoni, ukatili na umasikini"amesema.
Pareso,amesema takwimu zinaonesha zaidi ya wanafunzi 4,000 walikuwa wanakatisha masomo kutokana na changamoto hizo, hali iliyochochea maboresho ya sera ya elimu ili kuhakikisha hakuna mtoto anayekosa haki ya elimu.
Aidha amesema hadi sasa zaidi ya wanafunzi 10,000 wamerejeshwa shuleni, jambo ambalo linaonesha dhamira ya Rais Samia kuhakikisha watoto wote wanapata elimu bila ubaguzi.



