Na Avelina Musa - DODOMA.
Mbunge wa Viti Maalum wa kundi la wenye ulemavu, Stella Ikupa (CCM), amesema lugha ya alama inapaswa kufundishwa kama masomo mengine ya kawaida ili kila Mtanzania aweze kuwasiliana na watu wenye changamoto ya kusikia bila kutegemea wakalimani kila wakati.
Mhe Ikupa amesema hayo wakati akichangia mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ya mwaka 2026/2027 bungeni jijini Dodoma leo Mei 8, 2026, ambapo amesema hatua hiyo itarahisisha mawasiliano na kuongeza usawa wa upatikanaji wa elimu kwa watu wenye ulemavu, hususan wenye uziwi.
Amesema watu wenye ulemavu wa kusikia hukumbana na changamoto kubwa wanapohitaji huduma katika maeneo mbalimbali kama vituo vya polisi, hospitali, saluni na ofisi kutokana na uhaba wa watu wanaofahamu lugha ya alama.
“Endapo kila mtu atafahamu lugha ya alama, mawasiliano yatakuwa rahisi zaidi kwa watu wenye ulemavu wa kusikia,” amesema Ikupa.
Ametumia nafasi hiyo kuishauri Serikali kuwapa mafunzo ya elimu maalumu walimu wote nchini ili waweze kuwafundisha wanafunzi wenye mahitaji maalumu badala ya kutegemea kundi dogo la walimu waliobobea katika eneo hilo.
Aidha, ameomba shule maalumu na za mabweni zinazohudumia wanafunzi wenye ulemavu kuwa na wasaidizi maalumu watakaowasaidia wanafunzi hao katika shughuli za kila siku ili waweze kujifunza katika mazingira bora na salama.



