Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo imeiagiza Wizara ya Viwanda na Biashara kupitia Wakala wa Vipimo (WMA) kuanza kuhakiki vipimo vinavyotumika katika huduma za muda wa maongezi na bando za intaneti ili kuhakikisha wananchi wanapata thamani halisi ya fedha wanazolipia.
Kauli hiyo imetolewa leo Mei 22, 2026 na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kondoa Mjini, Mariam Ditopile, wakati akiwasilisha taarifa ya Kamati kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa mwaka wa fedha 2025/2026 pamoja na maoni ya Kamati kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Katika taarifa hiyo, Kamati imeeleza kuwa kumekuwepo na malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu uhalisia wa matumizi ya huduma za muda wa maongezi na bando za intaneti wanazonunua kutoka kwa kampuni mbalimbali za mawasiliano.
Kutokana na hali hiyo, Kamati imeishauri Serikali kuhakikisha Wakala wa Vipimo (WMA) unaanza rasmi jukumu la kuhakiki usahihi wa vipimo vinavyotumika katika huduma hizo ili kuimarisha uwazi na kulinda maslahi ya watumiaji.
Aidha,Ditopile, ameipongeza Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa shilingi bilioni 200 kwa ajili ya kuwawezesha vijana nchini.
