TFS YATOA MAFUNZO YA MFUMO MPYA WA UKUSANYAJI WA TAKWIMU ZA UZALISHAJI WA ASALI ILI KUONGEZA TIJA.

MUUNGANO   MEDIA
0

  



Na Avelina Musa - Dodoma.


KATIKA Kuinua Sekta ya Ufugaji wa Nyuki Nchini Wakala   wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umetoa mafunzo Maalum ya mfumo Mpya wa ukusanyaji wa takwimu za uzalishaji wa asali, hatua inayotarajiwa kuongeza uwazi, uaminifu na maendeleo ya sekta ya Nyuki Nchini Tanzania.


Hayo yamesemwa Leo November 20.2025 Jijini Dodoma na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa TFS, Hussein Msuya, wakati wa mafunzo hayo yenye lengo la kuwajengea uwezo wakusanyaji wa takwimu Kwa kubaini maeneo yenye uzalishaji mkubwa wa Asali, idadi ya wafugaji na fursa za uwekezaji katika sekta hiyo Nchini.



Kamishna Msuya amesema mafunzo hayo yatasaidia kuongeza maarifa  katika ukusanyaji wa takwimu za uzalishaji wa asali, hatua inayolenga kuboresha ubora wa taarifa za sekta ya ufugaji nyuki na kuongeza mchango wake katika uchumi wa taifa.

"Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa uzalishaji wa asali duniani,Ambapo kwa Bara la Afrika ni Nchi ya pili na taarifa sahihi za uzalishaji ni msingi muhimu katika kupanga na kuendeleza sekta hiyo."Amesema Kamishna Msuya.

Kwa upande wake, Mhifadhi Mkuu Frida Kundi kutoka makao makuu ya TFS, Kitengo cha Usimamizi wa Maendeleo ya  Rasiliamali za Maendeleo ya Ufugaji Nyuki amesema mafunzo hayo yanahusisha wataalam kutoka kanda saba za TFS nchini, ambao  baada ya mafunzo watakwenda kukusanya takwimu katika mikoa mbalimbali ili kubaini mwenendo wa sekta ya Ufugaji wa Nyuki Nchini.


 Amesema Takwimu hizo ni muhimu kwa Nchi na Taasisi katika kupanga mipango ya maendeleo, kusaidia jamii na kuongeza mchango wa sekta ya nyuki katika uchumi kwa TFS na zitasaidia hata katika kupata wataalam wa kuajiri kulingana na mahitaji ya sekta.

Hata hivyo Mtafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI), Stanislaus Lukiko amesema wameungana na TFS ili kuongeza utaalamu na kuhakikisha taarifa zinazokusanywa  ni sahihi na zinazoweza kutumika katika kupanga maendeleo ya sekta hiyo.



Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)