CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza kuwa kitachukua hatua kali dhidi ya viongozi wazembe na wanaojihusisha na vitendo vya rushwa na watakaoshindwa kwenda na Kasi ya utendaji wa Kiongozi wa Nchi.
Hayo yamesemwa Leo November 19 2025 Jijini Dodoma na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenan Kihongosi,ambapo amesema chama kitafuatilia utendaji wa viongozi katika ngazi zote ili kuhakikisha uwajibikaji unazingatiwa kikamilifu.
Amesema Mawaziri na Manaibu Mawaziri walioteuliwa na Rais wanapaswa kwenda na kasi ya utendaji wa kiongozi wa nchi huku akibainisha kuwa ingawa baadhi yao ni wapya na wanafurahia uteuzi, wanapaswa kufahamu kuwa Rais anataka kazi yenye matokeo kwa wananchi.
" CCM haitasita kumchukulia hatua yoyote atakayekwenda kinyume na maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan."Amesema Kihongosi.
"Viongozi wote Mawaziri, Manaibu Mawaziri, wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi na wengine wote walioteuliwa au kuchaguliwa wasiowajibika kwa wananchi, chama kitawawajibisha."Amesema.
Aidha, Kihongosi ametoa pongezi kwa uundwaji wa timu maalum ya kuchunguza vurugu zilizotokea October 29 mwaka huu pamoja na ahadi ya Rais ya kuanzisha mchakato wa Katiba Mpya ndani ya siku 100.
Akizungumzia umuhimu wa Amani Nchini,Kihongosi amesema amani ni rasilimali muhimu ambayo watanzania wanapaswa kuithamini na kuilinda kwa nguvu zao zote, huku akisisitiza kuwa taifa likipoteza utulivu madhara yake makubwa.
Amesema wapo watu ambao, kwa madai ya maslahi binafsi, wanaendesha kampeni za uchochezi kupitia mitandao ya kijamii kwa kuhamasisha vijana na baadhi ya wananchi kufanya vurugu na kuvuruga utulivu wa nchi.
"Nawaomba watanzania kuwakataa watu wa aina hiyo, kwa sababu wengi wao wanaishi nje ya nchi na kuwaacha vijana wa Tanzania kubeba mzigo wa madhara ya machafuko".Amesema Kihongosi.
MWISHO.
.jpg)