NGOs ZATAKIWA KUTUMIA FURSA YA DIRA YA TAIFA YA MAENDELEO.

MUUNGANO   MEDIA
0

 



Na Avelina Musa - Dodoma.


VIONGOZI  wa NGOs wametakiwa kutumia fursa ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 na Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano kuendeleza mchango wao katika sekta za afya, elimu, kilimo, maji, mazingira na uwezeshaji wananchi kiuchumi.


Hayo yameelezwa Leo Agosti 13, 2025 na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe Dkt. Dorothy Gwajima wakati alipomwakilisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Philip Isdori Mpango katika kilele cha Kongamano la Mwaka la NGOs Jijini Dodoma.

Dkt.Gwajima amesema  mashirika lazima yaendelee kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa miradi ya kijamii na kiuchumi sambamba na vipaumbele vya kitaifa.


Amesema ni ukweli usiopingika kuwa NGOs zimekuwa zikichagiza jitihada za Serikali katika kuwaletea Wananchi maendeleo kupitia utekelezaji wa miradi na afua mbalimbali hususani katika sekta ya afya, kilimo, elimu,maji, mazingira, utawala bora, ulinzi wa jamii,uwezeshaji wa jamii, miundombinu, mifugo na uvuvi pamoja na sekta nyingine mtambuka.


Katika kongamano hilo, Serikali ilipongeza mashirika kwa mchango wao katika kutoa ajira, kuboresha huduma za kijamii na kushirikiana katika mchakato wa ma preshow ya sheria, sera na miongozo ya sekta hiyo.

Aidha kuhusu Uchaguzi Mkuu wa 2025, NGOs zilizopewa vibali vya kutoa elimu ya mpiga kura na uangalizi wa uchaguzi zimetakiwa kufanya kazi kwa weledi na kuhamasisha wananchi kushiriki kwa amani na utulivu.


Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Bi. Hajjat Mwantumu Mahiza, amewaomba wanasekta hiyo kuendeleza mashirikiano kwaajili ya faida ya taifa na kizazi kijacho.

"Ndugu zangu hii nchi tinaijenga sote na kila mmoja ana dhamira njema kwa nchi yake, ni wasihi sana kila mmoja kwenye nafasi aliyopo kila unalolifanya tanguliza maslahi ya nchi kwanza, Tanzania hii ni yetu sote na inatutegemea na tunahitaji kuijenga Tanzania iwe mahali salama na penye neema nyingi kuliko tulivyoikuta sisi,"amesema.


 Naye Mwakilishi Mkazi wa  Umoja wa Mataifa Susan Namondo  amesema Umoja wa Mataifa utaendelea kufanya kazi kwa ukaribu na Serikali ya Tanzania kwa mwelekeo wa dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 ili kuweza kufanikisha yale ambayo nchi imedhamiria kuwafikia.

Mada kuu ya Kongamano hilo mwaka huu 2025 ni Tathmini ya Miaka mitano ya Mchango wa Mashirika Yasiyo Ya kiserikali katika Maendeleo ya Taifa 2020/21-2024/25: Mafanikio, Changamoto, Fursa na Matarajio.






Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)