Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, viongozi wa Dini wameendelea kutoa wito wa kudumisha amani nchini, wakisisitiza umuhimu wa maadili, mshikamano na kauli njema katika kipindi hiki
Akizungumza leo 8 Julai Jijini Dodoma Pastor Meshack Tulana Nhuti , anayehudumu katika Kanisa la Anglikana, Dayosisi ya Central Tanganyika, Parishi ya Nhalawanda Nzuguni B Kanisa la St . John Dodoma, amesema kuwa kanisa lina jukumu kubwa katika kuhubiri na kudumisha amani.
Sisi kama Kanisa tunahubiri amani. Pale tunapokosa kuhubiri amani, machafuko yanaweza kuingia. Kwa hiyo, tuhubiri amani katika kila hatua, kwa kila mtu
amesisitiza kuwa kila kiongozi wa dini anapaswa kuwa mfano wa kuigwa katika kulinda amani ya taifa.
“Sote ni wahubiri wa amani, iwe ni Kanisa Katoliki, Anglikana au makanisa ya Kipentekoste. Tunapaswa kuhubiri maneno yanayojenga na sio kubomoa,”
Aidha Pastor Meshack akizungumza kuhusu nafasi ya kanisa katika kulinda amani, amesema kuwa taasisi za kidini ni sauti kuu ndani ya jamii, hivyo kiongozi akisema jambo, watu wengi humsikiliza.
Ukihubiri chuki, watu watafuata chuki. Ukihubiri amani, watu wataenenda kwa amani. Tunapaswa kuwa na maadili, utu na kumcha Mungu, amesema
Katika kuelekea uchaguzi wa madiwani, wabunge na Rais, Pastor Meshack ametoa wito kwa Watanzania wote waliojiandikisha katika Daftari la Kudumu la Mpiga kura kujitokeza kwa wingi na kutimiza haki yao ya msingi ya kupiga kura na kumchagua kiongozi wako.
“Kura ni haki yako ya msingi. Tumia kura yako kuwachagua viongozi unaowaamini. Na wale walioamua kugombea, tunawaombea na kuwasihi kutumia lugha nzuri katika kampeni. Lugha ya matusi au kashfa haitujengi, bali inabomoa taifa,” amesema
Amewahimiza Vijana na kuwasihi kutumia nafasi zao kikamilifu katika ujenzi wa taifa na kanisa, amesema Taifa linawategemea.
“Nawatakia uchaguzi wenye amani, wenye furaha na upendo. Tuwe na Tanzania mpya yenye mshikamano,”
