HALI YA UCHUMI MKOA WA TABORA IMEIMARIKA KATIKA KIPINDI CHA UONGOZI WA AWAMU YA SITA.

MUUNGANO   MEDIA
0

 



Na Avelina Musa - Dodoma.


Mkuu wa Mkoa wa Tabora,Mhe. Paulo Chacha, amesema  hali ya Uchumi ya Mkoa wa Tabora imeendelea kuimarika ambapo Pato halisi la Mkoa limekua kutoka Shilingi Trilioni 5.4 mwaka 2020 hadi Shilingi Trilioni 6.3 mwaka 2024 sawa na ukuaji wa asilimia 17. Vilevile, pato la mtu mmoja mmoja limeongezeka kutoka shilingi milioni 1.77 mwaka 2020 hadi shilingi milioni 1.85 mwaka 2024 sawa na ongezeko la asilimia 4.5.


Amesema Mkoa wa Tabora umeendelea kupiga hatua kubwa katika sekta ya uzalishaji wa asali na uhifadhi wa mazingira, hali inayochochea maendeleo ya kiuchumi kwa wakulima na kuimarisha thamani ya asali ya Tabora kitaifa na kimataifa.


Mhe. Chacha amesema hayo Jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 11 2025 wakati akieleza mafanikio ya miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita kwa mkoa huo,  amesema,hadi kufikia mwaka 2025, viwanda vinne (4) vya kisasa vya kuchakata na kufungasha asali vimejengwa katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo kwa lengo la kuongeza thamani ya zao hilo.




 “Mwaka 2020 tulikuwa na uzalishaji wa asali tani 1,868.6, lakini sasa tumefikia tani 2,002.48 kwa mwaka 2025,hii ni hatua kubwa inayotokana na mikakati ya mkoa katika kuwajengea uwezo wafugaji wa nyuki na kuvutia uwekezaji kwenye sekta hii,” amesema Chacha.


Amesema  mafanikio hayo yameenda sambamba na juhudi za uhifadhi wa mazingira, ambapo misitu ya hifadhi ya vijiji imeongezeka kutoka misitu 6 yenye ekari 11,952.5 mwaka 2020 hadi misitu 37 yenye ukubwa wa ekari 330,780.75 mwaka 2025.


 “Kuongezeka kwa misitu ya hifadhi ya vijiji ni matokeo ya ushirikiano mzuri kati ya serikali, wananchi na wadau wa mazingira, hii inalinda vyanzo vya uzalishaji wa asali na kuongeza kipato kwa jamii,” ameeleza.


Aidha amesema Katika kipindi cha Uongozi wa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Mkoa umepokea jumla ya Shilingi Bilioni 34.9 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya vituo vya kutolea huduma za Afya.


"Mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kuimarika kwa miundombinu ya kutolea huduma za Afya, kuongezeka kwa upatikanaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi na kuimarika kwa upatikanaji wa huduma za Afya karibu na wananchi"Amesema Mhe Chacha.

Mhe.Chacha amesema kwa upande wa Sekta ya Elimu Idadi ya shule za msingi zimeongezeka kutoka 819 mwaka 2020 hadi 990 mwaka 2025 na idadi ya shule za sekondari zimeongezeka kutoka 197 mwaka 2020 hadi 264 mwaka 2025.



Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)