WABUNGE NA WADAU WA MICHEZO WAHAMASISHWA KUJENGA UTAMADUNI WA KUFANYA MAZOEZI.

MUUNGANO   MEDIA
0

 





Na Avelina Musa - Dodoma.



Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Wadau mbalimbali wa michezo, wamehamasishwa kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi ya mwili kwani yana umuhimu mkubwa si tu kwa afya bali hata kimahusiano baina yao, sambamba na kuongeza ufanisi kiutendaji. 


Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa alipokua akiwahutubia Wabunge na wadau hao baada ya kutamatika kwa michezo iliyoandaliwa na Benki ya CRDB kwa jina la ‘Bunge Grande Bonanza’ ambayo hufanyika kila mwaka, na mwaka huu limefanyika Juni 21, 2025 kwenye Viwanja vya Shule ya St. John Merlin Jijini Dodoma.



“Mazoezi haya tuliyoyafanya kupitia michezo hii na kupitia ‘Bunge Bonanza’ yana umuhimu mkubwa, si   tu kwa afya bali pia yanajenga urafiki miongoni mwetu, mahusiano mema miongoni mwetu ya kimichezo, lakini pia inaimarisha afya ya akili hivyo kuongeza ufanisi katika utendaji wa majukumu yetu ya kila siku katika maeneo yetu.”


Akizungumza kwa niaba ya Spika wa Bunge Mhe. Dkt. Tulia Ackson, Naibu Spika Mhe. Azzan Zungu, amesema Bonanza hili ni la mwisho kwa kipindi hiki ambacho Bunge linavunjwa na kwenda kwenye mchakato wa uchaguzi hivyo, amewashukuru Wadau wote waliohusika kwenye maandalizi ya shughuli hiyo.



“Wabunge hawa ni wenzetu, rafiki na ndugu zetu lakini pia tunafanya nao biashara hivyo wao ni sehemu ya jamii ya Dodoma. Kama tunavyofahamu Mhimili wa Bunge ulikuwepo muda mrefu hapa Dodoma na katika awamu hii tumebahatika kupokea Mihimili miwili ya nchi hii lakini wao wakiwa ni waanzilishi”.


Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bw. Abdulmajid Mussa Nsekela amesema, Benki yake inafanya mambo ya kijamii ndani na nje ya mipaka ya Tanzania kwani ndio utaratibu waliojiwekea kusaidia watu waliofikwa na majanga mbalimbali sambamba na kuandaa mabonanza ya michezo.


Aidha,Kamishna Generali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya  Bw. Aretas Lyimo, amesema wameshirikiana na Benki ya CRDB kuandaa Bonanza hilo kuelekea Maadhimisho ya siku ya Kupinga Matumizi ya Dawa za Kulevya Duniani kwani dawa hizo ni uhalifu wa kupangwa unaoharibu uchumi, ustawi wa jamii pamoja na vijana ambao ni nguvu kazi ya Taifa.


Benki ya CRDB imekua na utaratibu wa kudhamini Mabonanza ya michezo maarufu kama ‘Bunge Grande Bonanza’ kwa tangu mwaka 2021 ambalo hufanyika mara moja kwa mwaka katika mwezi Juni katikati ya Bunge la Bajeti ambapo mwaka huu lilianza kwa matembezi kutoka Chuo cha Mipango kuelekea Viwanja vya St. John Merlin na kupambwa na michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, mpira wa pete, kikapu, kukimbiza Kuku na mingine mingi.




Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)