Na Avelina Musa - Dodoma.
Imeelezwa kuwa katika kipindi cha miaka minne ya Uongozi wa Serikali ya awamu ya Sita, Serikali kupitia COSOTA imefanikiwa kusimamia ukusanyaji wa mirabaha na kugawa gawio kwa wasanii nchini.
Ambapo, katika kipindi hicho, jumla ya Shilingi 1,428,105,240.00 zimekusanywa kutokana na Tozo ya Hakimiliki (Copyright Levy), ambapo asilimia 60 ya fedha hizo, zitagawiwa kwa wasanii kama gawio la mirabaha mwezi Mei, 2025.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Habari, Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe, Prof. Palamagamba Kabudi leo Aprili 14,2025 wakati akieleza Mafanikio ya wizara hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Mhe,Prof. Kabudi amesema Serikali imefanikiwa kuhuisha na kuimarisha Tamasha la Serengeti Music Festival ambalo kwa sasa linajulikana kama Samia Serengeti Music Festival, ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Mheshimiwa Rais ya kuibua vipaji vya vijana, kukuza ajira na kutangaza utamaduni wa Taifa letu.
"Kwa mara ya kwanza, tamasha hili liliandaliwa mwaka wa fedha 2020/21 katika Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam. Tangu wakati huo, limeendelea kukua kwa kasi na kufanyika kwa mafanikio katika maeneo mbalimbali nchini, huku likiwa sehemu ya mkakati wa kuunganisha wasanii wa ndani na masoko ya kitaifa na kimataifa"Amesema Proff Kabudi.
Aidha kuhusu lugha ya Kiswahili amesema Katika kipindi kifupi cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita, Serikali imefanikiwa kutambua na kuenzi Kiswahili kama lugha muhimu kimataifa ambapo Serikali kupitia Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) imeratibu Kongamano la Kwanza la Kimataifa la Kiswahili, lililofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Havana, nchini Cuba, kuanzia tarehe 07 hadi 10 Novemba 2024.
" Hii ni baada ya tarehe 7 Julai kutambuliwa rasmi na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kama Siku ya Kiswahili Duniani," Amesema.
Kongamano hilo limekuwa na hatua muhimu katika kuimarisha Kiswahili kama lugha yenye umaarufu na umuhimu katika majukwaa ya kimataifa, na pia limeongeza utambulisho wa Tanzania duniani kote.
"Pamoja na kongamano hili, BAKITA lilizindua Kamusi ya Kiswahili - Kihispaniola, hatua ambayo imeendelea kukuza na kueneza Kiswahili," Amesema.
Hata hivyo Serikali ya Awamu ya Sita katika kipindi cha miaka minne, imefanikiwa kufungua vituo 19 vya kufundisha Kiswahili kupitia balozi za Tanzania katika nchi za Uholanzi, Abu Dhabi, Italia, Zimbabwe, Nigeria, Uswisi, Ufaransa, na Uturuki.
Mwisho.