Na Avelina Musa - Dodoma.
Waandishi wa Habari Nchini wametakiwa kutumia taaluma zao ili kufikisha elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa kupata huduma ya chanjo za magonjwa mbalimbali hususani chanjo ya Saratani ya Mlango wa kizazi.
Hayo yamesemwa na Afisa Program wa Mpango wa Taifa wa Chanjo Wizara ya Afya Bi. Lotalis Gadau wakati wa semina ya waandishi wa habari jijini Dodoma inayoenda sambamba na maadhimisho ya wiki ya chanjo yaliyoanza leo Aprili 24, 2025.
Afisa Gadau amesema chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi ilianzishwa baada ya kuona tatizo limekuwa kubwa hadi hapa tunapoongea takwimu zinaonesha kila mwaka wanawake 10,000,000 wanapata saratani ya mlango wa kizazi, kati ya hao 6,00,000 wanapoteza maisha.
“Wengi wetu hatuna deturi ya kufanya uchunguzi wa saratani hii, hivyo tunajua waandishi wa habari mnasikilizwa hivyo tunaomba mchukue fursa hiyo kupaza sauti kwa jamii ili wapate uelewa kuhusu saratani ya mlango wa kizazi,” amesema Bi. Gadau
Aidha Tanzania imeendelea kutekeleza utaratibu wa kutoa huduma za chanjo kupitia vituo vya kutolea huduma za afya 8500 vya Serikali na binafsi, kutekeleza huduma mkoba na tembezi ngazi ya jamii na mashuleni pamoja na kushirikiana na Wizara za kisekta ili kutoa huduma hizo mashuleni.
Hata hivyo kwa Upande wake Dkt. Tumaini Haonga Afisa kutoka Mpango wa Taifa wa Chanjo, Wizara ya Afya amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya imewafikia walengwa wa huduma za chanjo nchini kwa zaidi ya asilima 95 kwa kutekeleza na kuimarisha afua mbalimbali za chanjo.
Dkt.Haonga amesema kulingana na aina ya chanjo tunayoitoa na walengwa tunaohitaji tunakuwa na mikakati ya kuwafikia wananchi kwa maana ya wazazi, walezi na walengwa husika wa chanjo pale wanapopatikana kwa kuwatumia wahudumu wa afya ngazi ya jamii pamoja na wataalam wa afya kutoka kwenye zahanati zetu na vituo vya kutolea huduma za afya.
Maadhimisho wa wiki ya chanjo hufanyika kila mwaka mwishoni mwa mwezi Aprili ambapo kwa mwaka huu yameanza tarehe 24 hadi 30 Aprili, 2025 yenye kauli mbiu “Chanjo ni Kinga; Tuungane Kuwezesha Walengwa wote Wapate Chanjo”, kilele chake cha maadhimisho haya kitafanyika mkoani Tabora na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Afya Mhe.Jenister Mhagama.