TANZANIA YAWEKA MIKAKATI MADHUBUTI KATIKA TEKNOLOJIA YA AKILI UNDE - WAZIRI MKENDA.

MUUNGANO   MEDIA
0

 



_Na Mwandishi Wetu, Kigali -Rwanda.


 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia wa Tanzania, Mhe. Prof. Adolf Mkenda, amesema Tanzania imeongeza kasi katika kutumia na kuendeleza teknolojia ya Akili Unde (Ai) katika elimu kupitia utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Matumizi ya Teknolojia za Kidijitali.


Prof.Mkenda ameyasema hayo leo Aprili 04, 2025, alipowasilisha mada kuhusu ajira na nguvu kazi katika eneo la Akili Unde (Ai) wakati wa mjadala wa wadau wa elimu na teknolojia duniani, uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kigali (KCC),Nchini  Rwanda.


“Tanzania imeongeza kasi ya matumizi ya teknolojia za kidijitali ambayo ni dhamira ya Serikali ya Tanzania ya kuwawezesha vijana kupata mafunzo ya akili bandia na teknolojia zinazoibukia kupitia ufadhili wa masomo katika vyuo vikuu bora duniani”.


Prof. Mkenda amesema kuwa Serikali pia imeboresha Sera ya Taifa ya Elimu na Mafunzo pamoja na mitaala, kwa lengo la kuanza kuwajengea vijana uwezo wa TEHAMA ikiwemo Coding, kuanzia ngazi za chini za elimu


Aidha,Mjadala huo pia ulihusisha washiriki mashuhuri wakiwemo Waziri wa Elimu wa Rwanda, Mhe. Joseph Nsengimana, Mkurugenzi wa Uchumi wa Kidijitali kutoka Mastercard Foundation, pamoja na wawakilishi kutoka China na sekta binafsi.


Kongamano hilo limekuwa jukwaa muhimu la kujadili mustakabali wa Afrika katika mapinduzi ya teknolojia ya Akili Unde (Ai), likilenga kuimarisha sera, elimu na uwekezaji unaolenga kizazi kijacho cha kidijitali.


Mjadala huo ni sehemu ya Kongamano la Akili Bandia Barani Afrika, lililohitimishwa Aprili 04,2025 na uliwaleta pamoja viongozi wa serikali, wataalamu wa teknolojia, na wadau kutoka sekta binafsi na mashirika ya kimataifa.

Mwisho.

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)