DAWASA YAFANIKIWA KUONGEZA UHIFADHI WA MAJI KATIKA MIAKA MINNE YA RAIS DKT.SAMIA.

MUUNGANO   MEDIA
0

 



Na Avelina Musa - Dodoma.


MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imejipanga kutekeleza miradi mbambali ya maji ili kukidhi mahitaji ya maji lita bilioni 2.1 kwa siku ifikapo mwaka 2050 ikiwa ni makisio ya mara tatu ya mahitaji ya maji lita milioni 685 ya hivi sasa kwa siku.


Hayo yamesemwa leo Machi 11,2025 Jijini Dodoma na Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA,Mhandisi Mkama Bwire,wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa mamlaka hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita.


Mhandisi Bwire amesema jitihada hizo zimesaidia kuongezeka kwa upatikanaji wa huduma ya majisafi kutoka wastani wa asilimia 89 hadi asilimia 93 na huduma ya usafi wa mazingira kutoka asilimia 25 hadi asilimia 45.


Amesema uwezo wa uzalishaji maji umeongezeka kutoka lita 520,000,000 kwa siku mpaka lita 534,600,000 kwa siku sawa na ongezeko la lita 14,600,000 kwa siku.


Mhandisi Bwire ameeleza kuwa ni lazima kuwe na mipango ya muda mrefu ya kukidhi mahitaji ya maji ya maeneo yanayohudumiwa na DAWASA kwani kwa sasa ni mita za ujazo 685.6 lakini kutokana na kasi kubwa ya ongezeko la watu pamoja na viwanda, mahitaji ya maji lazima yazingatiwe ndiyo maana DAWASA imeangalia mahitaji ya maji ya leo, ya miaka 10 ijayo, hadi ya mwaka 2050. 


Mha.Bwire amesema mtandao wa majitaka umeongezeka kutoka kilomita 450 hadi kilomita 519.4 sawa na ongezeko la kilomita 69.4 na idadi ya maunganisho ya wateja wa majisafi imeongezeka kutoka 343,019 hadi 455,720 sawa na ongezeko la wateja 112,701.


“Vilevile kutolewa kwa kibali cha kuanza maandalizi ya mradi mkubwa wa kutoa maji kutoka Mto Rufiji ambapo utatosheleza mahitaji ya maji hadi mwaka 2050, utekelezaji wa kuandaa michoro ya

mwisho (detailed design) pamoja na kuandaa nyaraka za manunuzi (bidding documents) umefikia asilimia 8,”amesema Mha.Bwire.


Mha.Bwire amesema katika kipindi cha kuanzia Julai 2021,DAWASA imeendelea na utekelezaji wa miradi zaidi ya 25 yenye thamani ya fedha za kitanzania Shilingi billioni 987.6.


Mwisho.

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)