Na Avelina Musa - Dodoma
NAIBU Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Dodoma Euginius Hazinamwisho amewataka watanzania kushiriki katika kuzuia vitendo vya Rushwa kwani mapambano dhidi ya Rushwa ni wajibu wa kikatiba.
Hazinamwisho amesema hayo leo Agosti 7,2024 wakati akitoa taarifa ya kipindi cha mwezi April Hadi June 2024 katika mkutano wake na waandishi wa habari ambapo amebainisha vipaumbele vya Taasisi hiyo kwa Mkoa wa Dodoma kwa kipindi cha Julai hadi Septemba 2024 ikiwa ni pamoja na kuelimisha Umma kwa makundi tofauti ya wadau kuhusu madhara ya Rushwa katika miradi na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajia kufanyika mwaka huu.
Amesema katika vipaumbele hivyo pia wamepanga kuongeza Kasi ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuziba mianya ya Rushwa na uvujaji unaoweza kujitokeza katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
"Pamoja na utekelezaji wa majukumu yetu ya kawaida pia tumejiwekea malengo ya kutekeleza vipaumbele vinavyolenga Kuzuia vitendo vya Rushwa visitokee"amebainisha.
Aidha amebainisha kuwa kuongeza Kasi ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuziba mianya ya Rushwa na ufujaji unaoweza kujitokeza katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Hazinamwisho amesema katika ufuatiliaji huo wamebaini kuwepo kwa mapungufu kadhaa katika miradi kumi yenye thamani ya jumla ya shilingi 3,142,928,282.00 ambapo mapungufu hayo ni pamoja na utumiaji wa nondo zilizochini ya kiwango, matumizi ya mbao hafifu katika utengenezaji wa milango.
Mwisho.