Wanafunzi wa kidato cha nne shule ya Sekondari Igamba iliyopo kata ya Igamba Wilaya ya Mbozi Mkoa wa Songwe baada ya kujengewa uelewa wa elimu ya usalama barabarani wameahidi kushirikiana na Jeshi la Polisi kutoa elimu hiyo.
Kauli hiyo imetolewa na kiongozi wa serikali ya wanafunzi wa shule hiyo Sheila Issa Agosti 12, 2024 baada ya kupewa elimu ya usalama barabarani na Koplo Njika Musa wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Songwe ambapo amewafundisha makundi ya alama na michoro ya barabarani, matumizi sahihi na salama kwa watembea kwa miguu pamoja na upande sahihi wa mtembea kwa miguu awapo barabarani.
Aidha, wanafunzi hao wameahidi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kutoa elimu ya usalama barabarani na kuwa mabalozi katika kutoa elimu waliyoipata kwa jamii ili kupunguza na kutokomeza ajali mkoani Songwe.