Na Avelina Musa - Dodoma.
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera,Bunge na Uratibu Mhe,Ummy Nderiananga amelipongeza Shirika la CARE Tanzania kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali katika kuhakikisha kila mtanzania anakuwa na maisha Bora.
Mhe,Ummy ameyasema hayo Leo Agosti 4.2025 wakati alipotembelea Banda la Shirika la CARE Tanzania katika Maonesho ya Kitaifa ya Wakulima na Wafugaji Nane Nane (88) yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni Jijini Dodoma.
Mhe, Nderiananga amesema, "CARE Tanzania mmekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha wakulima wadogo watanzania wanainuka kiuchumi kwa kupitia miradi yenu mbali mbali."
"Niwapongeze sana kwa kazi nzuri mnazozifanya kwa kuzifikia jamii zetu kupitia miradi yenu hakika mmewainua watu wengi "alisema Nderiananga.
Kwa Upande wake Meneja Mwandamizi Shirika la CARE Tanzania Alfei Daniel Maseke amesema lengo la shirika hilo ni kusaidia kupunguza umaskini kwa watu wote hasa vijana na wanawake.
Maseke amesema shirika la CARE Tanzania linaendelea kutekeleza miradi ya kimaendeleo katika mkoa wa Iringa, Njombe, Tanga, Mbeya, Dar es Salaam, Morogoro, Singida na Zanzibar. Utekelezaji huo unaenda sambamba na mpango mkakati wa CARE Tanzania wa miaka mitano uliozinduliwa mwaka 2023. Mpango mkakati huo unalenga kuboresha maisha ya mtanzania kwa kuzingatia masuala ya usawa wa kijinsia, mabadiliko ya tabianchi, kukuza kipato kwa vijana na wanawake, lishe bora, afya njema na kutoa misaada pindi majanga yanapotekea kwenye jamii.
Aidha Barnabas Mtelevu Meneja Mwandamizi wa Mradi wa Pesa yake maisha yake unaotekelezwa Tanga, Njombe na Mbeya amesema lengo la mradi wa Pesa yake maisha yake ni kuboresha mnyororo wa thamani kwenye zao la Chai na viungo pamoja kukuza kipato cha mkulima mwanamke katika zao hilo.
Mwisho.