MGODI WA GGM WAANZA KUTUMIA UMEME WA GRIDI BADALA YA MAFUTA

MUUNGANO   MEDIA
0



Dkt.Biteko azindua kituo cha kupoza umeme cha GGM (MW 34)


 Asema kitaongeza mapato ya mgodi kwa Serikali


Aipongeza GGM kuzipa kipaumbele kampuni za kizawa


 TANESCO kuingiza mapato ya sh.Bilioni 2 hadi 3 kwa mwezi


 Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko

amezindua kituo cha kupokea na kupoza umeme katika Mgodi wa Dhahabu wa

Geita (GGM) chenye uwezo wa megawati 34 ambacho sasa kinawezesha GGML

kuanza kutumia umeme wa gridi kwa matumizi yake badala ya mafuta na

hivyo kupunguza gharama za uendeshaji.


Baada ya kuzindua kituo hicho tarehe 13 Agosti 2024 wilayani Geita

mkoani Geita, Dkt.Biteko amesema ujenzi wa kituo hicho ni alama

halisi ya umoja na ushirikiano uliopo kati ya Serikali na Sekta

Binafsi kwani mradi huo umehusisha ujenzi wa laini ya umeme ya kV 33

ambayo imejengwa na TANESCO kwa gharama ya shilingi bilioni 8.04 huku

GGML ikijenga kituo cha kupoza umeme kwa gharama ya Dola za Marekani

milioni 24.


Amesema GGM ilikuwa inatumia shilingi bilioni 130 kwa mwezi kama

gharama za uendeshaji na kwenye umeme wa mafuta ilikuwa inatumia

shilingi bilioni 13.4 kila mwezi na kuathiri mapato yake kwa Serikali,

hivyo kuanza kazi kwa kituo hicho kunapunguza gharama za uendeshaji

kwa mgodi na kupelekea Serikali kuongeza mapato yake, kuongeza ajira

na pia GGM kuweza kutanua shughuli zake.


Dkt.Biteko ameipongeza kampuni hiyo kwa kuanza kutumia umeme wa gridi

ambao unapunguza gharama za uendeshaji ambapo ametoa angalizo kuwa,

kupungua kwa gharama hizo kuguse pia watumishi kwa kuboresha maslahi

yao.


Ameeleza kuwa, umeme mwingi unaozalishwa kwa sasa unatoa uhakika wa

kwenda kwa wananchi na walaji wakubwa kama GGM na kuweka mkazo kuwa,

hayo ni matokeo ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuijali sekta

binafsi.


Vilevile, ameipongeza GGM kwa kuzipa kipaumbele kampuni za kizawa

katika kutoa huduma kwenye mgodi huo na kusisitiza kuwa huo ndio

msimamo wa Serikali ya Tanzania wa kuhakikisha kampuni za ndani

zinapewa kipaumbele kwenye miradi mbalimbali.


Dkt. Biteko amewaagiza Watendaji wa Wizara ya Nishati, TANESCO na

Taasisi nyingine za Serikali kujali sekta binafsi kutokana na manufaa

yake ikiwemo kuwa walipakodi wakubwa na kuongeza ajira nchini.


Pia, amewashukuru watangulizi wake katika Sekta ya Nishati, Dkt.

Medard Kalemani na January Makamba ambao katika kipindi chao

wakihudumu kama Mawaziri wa Nishati waliusimamia mradi huo ipasavyo.


Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio amesema

hali ya umeme nchini kwa ujumla ni nzuri huku uzalishaji ukikidhi

mahitaji na ziada kidogo.


Kuhusu usambazaji umeme mkoani Geita amesema kuwa Mkoa una Vijiji 486

na kati ya hivyo vijiji 483 vina umeme sawa na asilimia 99.38.


Ameongeza kuwa, kazi ya kupeleka umeme vitongojini mkoani Geita

inaendelea ambapo kati ya vitongoji 2,197, vitongoji takriban 1000

tayari vina umeme.


Ameongeza kuwa, Mkoa wa Geita umetengewa Shilingi bilioni 8.5 kwa

ajili ya kupeleka umeme maeneo ya migodi na viwanda na utekelezaji

umefikia asilimia 41.


Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella amemshukuru

Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira mazuri ya

uwekezaji nchini ambayo yamepelekea wawekezaji kufanya kazi na kuletea

nchi faida akitolea mfano kuwa, katika kipindi cha miaka mitatu GGM

imezalisha tani 51 za dhahabu ambayo ni mafanikio makubwa

yanayochangia ukuaji wa pato la Taifa.


Amemshukuru Rais Samia kwa kuwezesha umeme kufika pia kwenye migodi

ya Wachimbaji wadogo ambapo katika kipindi cha miaka mitatu wachimbaji

wadogo 19 wamepelekewa umeme kwenye migodi yao na kuwezesha uzalishaji

wa kilo za dhahabu takriban 11,000.


Wabunge mbalimbali waliohudhuria hafla hiyo wamempongeza Rais Samia

pamoja na uongozi wa Wizara ya Nishati kwa kutekeleza mradi huo ambao

una umuhimu mkubwa kwa uchumi wa nchi na mgodi wenyewe.


Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mha.Abubakari Issa

amesema kuzinduliwa kwa kituo hicho kutaiwezesha GGML kuanza kutumia

umeme wa gridi kwenye matumizi yake pamoja na kuongeza mapato ya

TANESCO ambapo inategemewa yataongezeka kwa kiasi cha shilingi bilioni

2 hadi 3 kwa mwezi.


Makamu wa Rais wa kampuni ya Anglo Gold Ashanti-Tanzania

anayeshughulikia Miradi Endelevu, Simon Shayo ameishukuru Serikali

kwa kuweka mazingira mazuri ya biashara na miundombinu madhubuti ya

umeme inayowawezesha kufanya biashara kwa ufanisi.


Amesema mradi huo ni muhimu kwa GGM kwani unawawezesha kupata umeme wa

gridi na kupunguza matumizi ya umeme wa mafuta ambapo gharama

zitapungua kwa asilimia 92.


Viongozi mbalimbali waliohudhuria hafla hiyo ni Wenyeviti na Makamu

Wenyeviti wa Kamati mbalimbali za Bunge, Wabunge kutoka Mkoa wa Geita,

Watendaji kutoka Wizara ya Nishati, Shirika la Umeme Tanzania (

TANESCO) na GGM.



Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)