Naibu
Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Christina Mndeme akiwa
katika picha ya pamoja na wadau mara baada ya kufungua Kikao kazi cha Wadau cha Kukusanya Maoni Kuhusu Rasimu ya Mpango Kazi wa Taifa wa
Masuala ya Jinsia na Mabadiliko ya Tabianchi jijini Dodoma tarehe 19 Julai, 2024.
Na.Mwandishi wetu
Naibu
Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Christina Mndeme ametoa
wito kwa wadau wa mazingira kuwekea mkazo suala la nishati safi ya kupikia
katika Rasimu ya Mpango Kazi wa
Taifa wa Masuala ya Jinsia na Mabadiliko ya Tabianchi.
Bi. Mndeme amesema hayo
amesema hayo wakati akifungua Kikao kazi cha Wadau cha Kukusanya Maoni Kuhusu Rasimu ya
Mpango Kazi wa Taifa wa Masuala ya Jinsia na Mabadiliko ya Tabianchi, jijini Dodoma leo tarehe 19 Julai, 2024.
Amesema athari za mabadiliko ya tabianchi sekta za
kiuchumi ambazo wanawake, wanaume, watoto, wazee,
vijana na makundi maalum hutegemea kwa maisha yao ya kila siku.
Bi. Mndeme amesema sababu mbalimbali zikiwemo majukumu yao kijinsia,
utamaduni, umri, uchumi, mila na desturi huchangia makundi hayo ya jamii
kuathirika na athari za mabadiliko ya tabianchi.
“Hii ni hatua kubwa katika uwezeshaji wa masuala ya jinsia hapa nchini, kama
mnavyofahamu, Tanzania ni Mwanachama wa
Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, Itifaki ya Kyoto na
Makubaliano ya Paris. Makubaliano ya Paris yanazitaka Nchi Wanachama kuandaa
Mpango Kazi wa utekelezaji wa Programu ya Lima kuhusu masuala ya Jinsia na
Mabadiliko ya tabianchi,” amesema.
Itakumbukwa kuwa Mkataba huo ulianzishwa mwaka 2014 katika mkutano wa 20 wa
Nchi Wanachama wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP20) uliofanyika Lima nchini Peru.
Madhumuni ya LWPG ni kuzihimiza nchi Wanachama wa Mkataba kuhuisha masuala ya
jinsia katika mipango kazi ya kitaifa ili kutekeleza Mkataba na Makubaliano ya
Paris. Hivyo, Ofisi ya Makamu wa Rais kama Ofisi Kiungo wa Mkataba wa
Mabadiliko ya Tabianchi nchini, inaratibu maandalizi ya Mpango Kazi husika.
Hata hivyo, Bi. Mndeme amesema tafiti zimeonesha nchi zinazoendelea bado
hazijahuisha Programu ya Lima katika mipango, sera na mikakati ili kuwezesha
kuwa na takwimu za makundi hayo, usawa wa kijinsia, uwezeshaji wanawake
katika majadiliano ya kimataifa, uhuishaji wa masuala ya jinsia katika
sera, mipango na mikakati ya Taifa na kujenga uwezo wa kifedha,
utaalam, fedha na taasisi katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Serikali tayari imehuisha masuala
ya Jinsia na Mabadiliko ya Tabianchi katika Sera ya Taifa ya Mazingira (2021),
Mpango Kabambe wa Mazingira (2022-2032), Mkakati wa Taifa wa Mabadiliko ya Tabianchi
(2021-2026) na Mchango wa Taifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi
(2021-2026). Hivyo, maandalizi ya Mpango Kazi wa Taifa wa Masuala ya Jinsia na
Mabadiliko ya Tabianchi ni mwendelezo ya Jitihada za Serikali katika
kukabiliana na mabadiliko ya tabainchi kwa kwa makundi yote ya kijamii ili
kuweza kuleta maendeleo endelevu hapa nchini.